KWA kawaida binadamu yeyote huzaliwa na kubatizwa jina ambalo hulitumia katika masomo na hata kazi yake.
Tofauti na ilivyo katika fani nyingine, wasanii wamekuwa wakijibatiza majina ya ziada (a.k.a). Mbaya zaidi, majina hayo huwa yanaanza kama utani lakini inafika wakati msanii husika
analizoea jina hilo jipya na kulifanya kuwa kama rasmi. Leo Amani linakuletea orodha ya baadhi ya mastaa ambao majina waliyopewa na wazazi wao ‘yamekufa’, hawayatumii kabisa: LULU
Jina lake halisi ni Elizabeth Michael, Lulu lilizoeleka kupitia tasnia ya uigizaji. Alianza kulitumia wakati alipojiunga na Kundi la Sanaa la Kaole.
Hadi leo hii, siyo rahisi kabisa mtu kutokea na kumuita jina la Elizabeth, wengi wanamfahamu kwa jina la Lulu.
RAY
Ray ndiyo jina ambalo limezoeleka na wengi. Vincent Kigosi alilopewa na wazazi wake ni kama limekufa. Kwa zaidi ya miaka kumi sasa tangu alipokuwa kwenye Kundi la Sanaa la Kaole hadi sasa.
Jina la Ray ndiyo watu wanalolifahamu zaidi ingawa hivi karibuni baadhi ya wasanii wenzake wamekuwa wakijaribu kumuita Vincent ili kurudisha uhai wa jina hilo.
JOHARI
Jina lake halisi ni Blandina Chagula. Johari lilizaliwa kwenye Tamthiliya iliyobeba taito ya jina hilo. Akiwa katika Kundi la Kaole, alianza kujiita Blandy, baadaye alibadilisha jina hilo na kuwa Johari walipoingiza tamthiliya hiyo ambayo pia ilizaa filamu.