POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imebaini kuwa chombo
kilichodhaniwa kuwa bomu katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), Usharika wa Kijitonyama hakikuwa bomu, bali ni kifaa cha
Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) cha kuchunguza anga.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleman Kova alisema hayo jana alipozungumza na waandishi
wa habari, baada ya kufanya uchunguzi kwa kushirikiana TMA.
"Baada ya kupata taarifa, polisi walifika eneo la tukio na
kukuta kifaa kilicho katika umbo la kasha kikining'inia kwenye transfoma
karibu na Kanisa kikiwa kinawaka taa.
“Katika kasha hilo kulikuwa na maandishi ya kalamu ya wino yaliyosomeka TMA na Airport," alisema Kamanda Kova.
Alisema baada ya uchunguzi wa awali, polisi walibaini kuwa
kifaa hicho si bomu na kuondoka nacho kwa uchunguzi zaidi. Mtabiri
Mwandimizi wa hali ya hewa kutoka TMA, Augustino Kanemba, alisema kifaa
hicho kinaitwa Radio Sound na hutumiwa na Mamlaka hiyo kufanya utafiti
wa hali ya anga za juu.