Msanii wa Hip Hop na mshindi wa tuzo 3 za KTMA 2013, Kala Jeremiah amefunguka kwa kuandika waraka mrefu kuelezea jinsi anavyomkubali waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa kwamba anafaa kuiongoza nchini.
Usome waraka wake huo wote;
Mimi Kala Jeremiah nilikuwa msanii wa kwanza Tanzania kumsema mheshimiwa Edward Lowassa kupitia wimbo wangu uitwao wimbo wa taifa baada ya mheshimiwa kukumbwa na kashfa ya ufisadi wa Richmond.
Kwa kipindi kile kila mmoja wetu alihamaki sana na kuona kweli mzee wa watu ni fisadi.Kwenye wimbo huo kuna mistari nilisema, ‘mi siyo mwana siasa sisubiri tume ichunguze nistaafu ka Lowassa.
Kwa kuwa mimi ni mzuri sana kwenye kufanya uchunguzi binafsi nilitumia muda mwingi sana kulichunguza swala hili la kashfa hii na baadae niligundua kuwa ni swala la kisiasa, na yalikuwa ni mapito ambayo mwanadamu yoyote hupewa muda wa kupitia magumu ili kupimwa imani yake kwa Mungu.
Baada ya kugundua hayo mwaka jana nilitengeneza wimbo unaoitwa ‘Azimio la Arusha’ ambao upo kwenye album yangu ya Pasaka ambayo iko sokoni tokea mwaka jana.