Wakazi wa jiji la Dar es Salaam, wameambiwa wachukue tahadhari na umakini wakati wa kununua samaki nyakati za jioni, kutokana na madai kuwa baadhi ya wachuuzi huvua kwa kutumia mabomu.
Tahadhari hiyo imekuja baada ya kufanya uchunguzi wa muda mrefu, ambapo imegundua samaki hao wanauzwa nyakati hizo kukwepa kugundulika.
Imefahamika licha ya Serikali kuwa na kampeni ya kusaka watu wanaojihusisha na uvuvi huo, bado hali imekuwa mbaya katika maeneo ya pwani ya bahari ya Hindi.
Maeneo yanayotajwa kukithiri kwa uvuvi wa mabomu ni Pwani ya Bagamoyo, Kawe katika Manispaa ya Kinondoni na Buyuni eneo la Kigamboni, Manispaa ya Temeke.
Baadhi ya wavuvi waliofanikiwa kuzungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yao kwa usalama, walisema watu wanaojihusisha na uvuvi haramu wanatumia mbinu nyingi za kuingiza samaki sokoni.
Walisema watu wengi kutokana na kuanza kuwabaini samaki wa aina hiyo, wavuvi wanawauza kwenye maeneo ya mikusanyiko ya watu nyakati za jioni bila ya kugundulika kwa urahisi.