RAIS Jakaya Kikwete
amesimulia maisha yake ya jeshini, huku akikumbuka namna alivyokamatwa
na mkuu wa jiko (afande ubwabwa) akiiba wali. Rais Kikwete alitoa
ushuhuda huo wakati akifunga mafunzo maalumu ya uongozi kwa wabunge na
kuzindua mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria.
Hafla
hiyo ilifanyika juzi katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)
kikosi cha 832 KJ, kilichopo Ruvu, Kibaha mkoani Pwani, ambapo viongozi
mbalimbali walihudhuria.
Rais Kikwete aliwakumbusha vijana hao
kwamba yeye ni miongoni mwa watu waliochukua mafunzo ya JKT kambini
hapo akiwa katika Operesheni Tumaini mwaka 1972.
Rais Kikwete
alisema katika mafunzo hayo alijengwa vizuri, ingawa hadi leo bado
anakumbuka matukio mawili ya kufurahisha na kusikitisha akiwa kambini
hapo.
Alisema tukio la kwanza ambalo hawezi kusahau ni pale
alipokamatwa akiiba wali na tukio jingine ni kuhusu kifo cha askari
mwenzao aliyefariki dunia baada ya kukanyagwa na trekta.
“Nawashukuru
kwa kunialika katika shughuli hii, nimetembelea na kujionea miradi
mbalimbali inayoendelea kufanywa hapa kambini.
“Wakati tukiwa kule nilikuwa naangalia
kwa makini, hasa nilikuwa naangalia lile bweni letu, sisi tuliokuwa
Kombania A mwaka ule, nimepakumbuka ingawa sasa pamekarabatiwa vizuri.
“Yapo
matukio mawili ninayoyakumbuka siwezi kuyasahu hadi leo wakati nikiwa
hapa kambini…(kicheko) jeshi si mchezo, nawaeleza haya mjue maisha ya
jeshi hayana mzaha.
“Nakumbuka namna nilivyokamatwa na bwana
ubwabwa nikiiba wali kule katika bwalo la chakula,” alisema Rais
Kikwete huku wananchi na askari wanafunzi (kuruta) waliokuwapo
wakiangua kicheko.