RAIS Jakaya Kikwete
amesimulia maisha yake ya jeshini, huku akikumbuka namna alivyokamatwa
na mkuu wa jiko (afande ubwabwa) akiiba wali. Rais Kikwete alitoa
ushuhuda huo wakati akifunga mafunzo maalumu ya uongozi kwa wabunge na
kuzindua mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria.
Hafla hiyo ilifanyika juzi katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikosi cha 832 KJ, kilichopo Ruvu, Kibaha mkoani Pwani, ambapo viongozi mbalimbali walihudhuria.
Rais Kikwete aliwakumbusha vijana hao kwamba yeye ni miongoni mwa watu waliochukua mafunzo ya JKT kambini hapo akiwa katika Operesheni Tumaini mwaka 1972.
Rais Kikwete alisema katika mafunzo hayo alijengwa vizuri, ingawa hadi leo bado anakumbuka matukio mawili ya kufurahisha na kusikitisha akiwa kambini hapo.
Alisema tukio la kwanza ambalo hawezi kusahau ni pale alipokamatwa akiiba wali na tukio jingine ni kuhusu kifo cha askari mwenzao aliyefariki dunia baada ya kukanyagwa na trekta.
“Nawashukuru kwa kunialika katika shughuli hii, nimetembelea na kujionea miradi mbalimbali inayoendelea kufanywa hapa kambini.
“Wakati tukiwa kule nilikuwa naangalia kwa makini, hasa nilikuwa naangalia lile bweni letu, sisi tuliokuwa Kombania A mwaka ule, nimepakumbuka ingawa sasa pamekarabatiwa vizuri.
“Yapo matukio mawili ninayoyakumbuka siwezi kuyasahu hadi leo wakati nikiwa hapa kambini…(kicheko) jeshi si mchezo, nawaeleza haya mjue maisha ya jeshi hayana mzaha.
“Nakumbuka namna nilivyokamatwa na bwana ubwabwa nikiiba wali kule katika bwalo la chakula,” alisema Rais Kikwete huku wananchi na askari wanafunzi (kuruta) waliokuwapo wakiangua kicheko.