Harakati za
kuwania urais ndani ya CCM zimeingia katika hatua mpya baada ya
mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale - Mwiru kuibuka na kudai kuwa wote
waliojitokeza kuwania nafasi hiyo hawana sifa kwa kuwa wanatumia fedha
kutaka kuingia Ikulu.
Kauli ya mwanasiasa huyo ambayo imekuja siku moja
kabla ya Kamati Kuu ya CCM kukutana leo mjini Unguja na moja ya ajenda
ikitajwa kuwa suala la maadili, inaweza kuwa mwiba mchungu kwa wanasiasa
hao ambao wanaongezeka kila kukicha.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kingunge alisema:
“Kuna suala la kukosa uadilifu, kuna suala la matumizi ya pesa na
nikwambie ukweli, hao wanaotangaza urais wote wanatumia pesa, wanatumia
faulo mbalimbali na wananchi wanajua.” Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Kwa miezi kadhaa sasa, baadhi ya makada wa CCM
wamekuwa wakitajwa kufanya harakati kichinichini na wengine kushiriki
shughuli za wazi zinazoashiria kuwa wanataka kuwania nafasi hiyo ya juu.
Hadi sasa makada wanne tayari wameweka wazi nia yao hiyo.
Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, January Makamba kwa nyakati tofauti walitoa kauli
zinazowashutumu makada wengine wa chama hicho kwa matumizi makubwa ya
fedha katika kushawishi uungwaji mkono.
Hata hivyo, kauli za wanasiasa hao zimedaiwa kuwa
ni fitina za kisiasa kwa kuwa wagombea wote wanatoa fedha, bali
wanazidiana viwango tu.
Mbali na Makamba na Membe, wanaCCM wengine
waliotangaza au kutajwa kuwania urais ni Mbunge wa Nzega, Dk Khamis
Kigwangalla, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda.
Wengine ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward
Lowassa na Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Uratibu), Stephen Wasira na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini,
William Ngeleja.
Kauli ya Kingunge aliyoitoa kupitia Televisheni ya
ITV, imekuja wakati wanasiasa sita miongoni mwa hao wanaotajwa
wakikaribia kumaliza miezi 12 ya uangalizi kutokana na onyo kali dhidi
yao lililotolewa na Kamati Kuu ya CCM Februari 18, mwaka jana baada ya
kuwatia hatiani kwa makosa ya “kuanza kampeni mapema na kufanya mambo
ambayo ni kinyume na maadili ya chama na ya jamii.”
Wanaotumikia adhabu hiyo ni Lowassa, Sumaye, Njeleja, Makamba, Wasira na Membe.
Akisisitiza hoja yake hiyo bila kutaja majina,
Kingunge alisema makada hao wamekuwa wakitumia fedha nyingi kujitangaza
na kutengeneza ushawishi wa kukubalika kwa wananchi jambo ambalo ni
kinyume na maadili ya uongozi.
Kingunge alisema mwanasiasa yeyote anayehitaji uongozi hapaswi kutumia fedha kushawishi wananchi wamchague. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Na Mwananchi
“Kiukweli tukiangalia wote wanaojitangaza hakuna msafi hata
mmoja... hatuwezi kuchagua rais kama vile tunachagua wachezaji wa mpira,
haiwezekani. Tunataka kupata mgombea wa urais ambaye atakuwa na uwezo
wa kushughulikia kwa vitendo kero na umaskini wa Watanzania,” alisema
Kingunge.
Alisema badala ya viongozi kutumia muda mrefu
kumtafuta mchawi, ni vyema wakatazama namna ya kushughulikia suala la
maadili kwa sababu kati yao hakuna msafi hata mmoja.
Kuhusu watu wengi kujitokeza kutaka urais,
Kingunge alisema: “Kujitokeza kugombea urais siyo dhambi, ingawa watu
wanashangaa kidogo kwamba kila mtu anaibuka tu anataka urais, kidogo
inaleta kasoro lakini siyo kitu, wanataka kutumia haki zao.”
Mkongwe huyo wa siasa alisema wananchi ndiyo
wanaowajua wagombea hao na sifa zao, hivyo wakumbuke kuwa anayechaguliwa
ni rais na siyo mchezaji wa mpira.
“Mnachagua rais ambaye ataweza kuwaunganisha kama
Taifa, ataweza kuwatumikia kwa vitendo siyo kujitumikia wenyewe, pia
ataweza kutatua matatizo yanayowakabili wananchi,” alisema.
Aliongeza kwamba kwa kuwa tatizo kubwa la wananchi ni umaskini, wananchi watazame mtu atakayeweza kuondoa hali hiyo.
Akizungumzia kuhusu namna viongozi wa Afrika
wanavyoyatumia madaraka yao, Kingunge alisema wamepiga hatua kubwa
lakini bado haitoshi kwa kuwa wanakosa namna chanya ya kutumia madaraka
ambayo Afrika iliyapigania kutoka kwa wakoloni.
“Tumeupigania uhuru ili tuendeshe nchi yetu
wenyewe, turudishe ile thamani yetu kama watu. Sasa madaraka tumepata,
lakini tunayatumiaje?” alihoji.
Kuhusu Mapinduzi
Kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar yaliyotimiza miaka 51 jana, Kingunge alisema yamekuwa na faida kubwa kwa Wazanzibari.
Alisema Mapinduzi hayo ndiyo msingi wa Muungano
ambao umeleta mafanikio makubwa kwa pande zote licha ya changamoto
zinazoibuliwa.
“Haikuwa na budi kufanya mapinduzi kwa kuunda kamati ya wapiganaji 14
ambao waliongoza kazi hiyo baada ya kuona mfumo uliokuwa unatumiwa na
Serikali ya Sultan unawakandamiza wazawa. Baada ya mapinduzi hayo
kufanikiwa, ardhi iliyokuwa inamilikiwa na kundi moja la Waarabu
ikagawanywa kwa kila Mzanzibari akapata ekari tatu, pamoja na hali hiyo
elimu ilitangazwa kutolewa bure.” Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment