Polisi
nchini Kenya wamewahoji maafisa wakuu watendaji wa kampuni za huduma za
simu za rununu kuhusu usajili wa kadi za simu za mkononi zinazotumia
huduma za kampuni hizo.
Hatua ya polisi imefuatia ripoti kuwa
simu zenye kadi ambazo hazikuwa zimesajiliwa zilitumiwa na magaidi
walioshambulia jumba la Westgate mjini Nairobi wiki mbili zilizopia.
Wanne hao walitishiwa kukamatwa mnamo
siku ya Jumatatu baada ya maafisa wa serikali kuwatuhumu kwa kuuza kadi
za simu ambazo hazijsajiliwa.
Hata hivyo walikana tuhuma hizo.
Mnamo mwaka 2010, serikali ya Kenya
ilieleza kuwa sharti mmiliki wa simu kusajili kadi yake ya simu ya
mkononi katika hatua ya serikali kuzuia visa vya uhalifu wa kutumia simu
za mkononi. Hata hivyo sheria ilianza kutekelezwa mwaka jana.
Takriban watu 67 waliuawa kwenye
mashambulizi hayo na wengine wengi kujeruhiwa kwenye mashambulizi
yaliyofanywa na kundi la kigaidi la al-Shabab .
Katika taarifa yao ya pamoja, maafisa
hao wakuu wa kampuni za huduma za simu,Safaricom, Bharti Airtel, Orange
Kenya na Yu Essar – walisema kuwa walitoa taarifa kwa polisi asubuhi ya
leo.