Kumekuwa na kelele za waumini nchini Ujerumani wakishinikiza askofu huyo afukuzwe kwa kukiuka taratibu.
Vatican City. Makao Makuu ya Kanisa
Katoliki Duniani (Vatican) yamemsimamisha kazi Askofu wa Jimbo la
Limburg, Ujerumani Franz-Peter Tebartz-van Elst anayekabiliwa na kashfa
ya matumizi mabaya ya fedha kwa shughuli za kifahari.
Vatican ilieleza jana kuwa uamuzi huo
umechukuliwa baada ya kuridhika kuwa Askofu van Elst amekiuka maadili
yaliyowekwa na Papa Francis kwa viongozi walioko chini yake akiwataka
waishi maisha ya uchaji, umaskini.
Hadi sasa, kumekuwa na kelele nyingi miongoni mwa waumini nchini Ujerumani wakitaka askofu huyo afukuzwe kazi.
Miongoni mwa matumizi yake makubwa ni
ujenzi wa makazi yake binafsi yaliyogharimu Euro 2.9 milioni (Dola 3.9
milioni), ukumbi wa chakula wenye mita za mraba 63 ambao ni pamoja na
mesi na bafu yenye thamani ya Euro 15,000.