Hali ya usalama katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani hapa imezidi kuwa mbaya baada ya askari polisi kudaiwa kufanya unyama kwa kuwabaka wanawake na kumpiga risasi mjamzito
Mbali na unyama huo polisi pia wanadaiwa kuchoma moto nyumba tatu za wananchi katika mtaa wa Magomeni na vibanda vya maduka kadhaa na kupora vitu vilivyomo ndani.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa anasema hali ni shwari na kwamba wananchi watoke nje kuendelea na shughuli zao kama kawaida.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamedi Kodi amethibitisha kupokea mwili wa mjamzito ukiwa na tundu tumboni, zinazoaminika kuwa za risasi na hivyo kufanya idadi ya maiti zilizopokelewa hospitalini hapo kufikia mbili na majeruhi 18: “Ni kweli kwa leo tumepokea maiti moja ya mwanamke ambaye ni mjamzito wa miezi saba, amepigwa risasi tumboni...” “...pia tumepokea mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Chuno, amevunjwa miguu yote kwa risasi.”