Tume ya Uchunguzi inayotarajiwa kukamilisha maelezo yake hivi karibuni, ilipewa hadidu za rejea ambazo ni kubainisha sababu za matokeo hayo mabaya, kubaini sababu za kushuka kwa kiwango cha ufaulu na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua.
Akijibu swali la papo kwa hapo la Mbunge wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya (CUF), Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema kinachosubiriwa sasa, ni maelezo ya kina ya Tume ya Taifa aliyoiunda kuchunguza matokeo hayo.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Tume hiyo haijakamilisha kazi yake, lakini muda si mrefu itakuwa imekamilisha na kuwasilisha maelezo ya kina yatakayoipa Serikali majibu kwa maeneo yote.
“Tusubiri kidogo, muda si mrefu tutakuwa tumekamilisha kazi …na kama wapo watu waliosababisha jambo hili, wala haitakuwa tatizo hata kidogo kuchukua hatua za kuwawajibisha. Ni dhahiri kwamba suala hili si dogo,”alisema Waziri Mkuu.
Majibu hayo ya Pinda yalitokana na maswali ya Mbunge Sakaya, ambaye alisema uamuzi wa Serikali wa kufuta matokeo hayo kutokana na kubainika kulikuwa na mabadiliko ya upangaji wa alama bila kuandaa wanafunzi, si jambo dogo.