Mwenyekiti
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe ametuma
salaam za rambirambi ya kifo cha Dkt. Edmund Sengondo Mvungi, akitoa
pole kwa familia, uongozi na wanachama wa NCCR-Mageuzi, Tume ya
Mabadiliko ya Katiba Mpya na wananchi wote walioguswa na msiba huo.
Akitoa kauli hiyo kwa niaba ya CHADEMA na wanachama wa chama hicho, Mwenyekiti Mbowe amesema kuwa amepokea kwa masikitiko
na mshituko mkubwa taarifa za kifo cha Dkt. Mvungi, akimwelezea kuwa
alikuwa mwanasiasa mwenye msimamo ambaye hakuwahi kutetereka kusimama na
chama chake tangu alipojiunga nacho na kuanza kushiriki siasa za
mageuzi nchini.
“Kwa niaba
ya CHADEMA na wanachama wetu nchi nzima, napenda kutoa salaam za pole
sana kwa familia ya marehemu, mjane na watoto. Natoa pole kwa Mwenyekiti
wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na wanachama wa chama hicho, pia tunatoa
pole kwa Jaji Mstaafu Joseph Warioba na makamishna wote wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kwakifo cha Dkt. Mvungi. Tunaomba Mwenyezi Mungu
awatie nguvu sana wakati huu wa majaribu na majonzi makubwa.
“Dkt.
Mvungi alikuwa mwanasiasa mwenye misimamo ambaye hakuwahi kukihama chama
chake tangu alipoanza siasa za mageuzi nchini. Ni kati ya wasomi
wachache waliokuwa na ujasiri na kuthubutu kujiunga na vyama vya
upinzani tangu mapema.
"Mvungi pia
alikuwa mmoja wa wanasiasa wa mwanzo kabisa kupigania nchi yetu iwe na
Katiba Mpya, ili hatimaye siasa zetu, hususan demokrasia ya vyama vingi
nchini iendeshwe kwa misingi iliyo imara,” amesema Mwenyekiti Mbowe na
kuongeza;
“Mwenyezi
Mungu alimjalia marehemu akaweza kushiriki kutimiza ndoto hiyo baada ya
kuteuliwa kuwa mmoja wa makamishna wa Tume ya Mpya, kazi ambayo
ameifanya hadi siku alipokutwa na tukio lililosababisha mauti yake.”
Mwenyekiti
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa
Hai, amesisitiza kuwa kwa namna ambavyo Dkt. Mvungi alikuwa mstari wa
mbele katika suala hilo, Tume ya Katiba Mpya inao wajibu wa kuthamini
mchango wake katika hatua iliyofikia sasa ya mchakato huo nyeti hadi
utakapofika mwisho.
“Wakati
tukimwombea marehemu kwa Mungu, alazwe mahali pema peponi, ni matumaini
yetu kuwa serikali kupitia vyombo vyake itahakikisha kuwa wale wote
waliohusika katika tukio la lililosababisha kukatisha uhai wa Dkt.
Mvungi wanapatikana na kuchukuliwa hatua zote zinazostahili kisheria,”
amesema Mwenyekiti Mbowe.
"Kwa masikitiko makubwa, Tume
inawafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake, Dkt. Sengondo Mvungi aliyekuwa
akipata matibabu katika Hospital ya Milpark iliyopo jijini Johannesburg
nchini Afrika Kusini amefariki dunia leo Jumanne, Novemba 12, 2013 saa
8:30 mchana kwa saa za Afrika ya Kusini," amesema Bwana Rashid katika
taarifa yake fupi.
Amesema taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka nchini Afrika Kusini kuja nchini Tanzania kwa mazishi zinaendelea.
Marehemu Dkt. Mvungi alisafirishwa
siku ya Alhamisi, Novemba 7, 2013 kwenda nchini Afrika Kusini kwa
uchunguzi na matibabu zaidi akitokea Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI)
alipokuwa amelazwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake.
Dkt. Mvungi pamoja na kuwa ni
mwanasheria aliyebobea katika fani ya Katiba, pia ni mwanasiasa ambaye
aliwahi kugombea urais mwaka 2005 kupitia chama cha NCCR Mageuzi.