Tuesday, March 01, 2016

DAKTARI ASIMAMISHWA KAZI KISA LAKI MOJA

Baada ya kufichua uozo katika bandari tatu kubwa hapa nchini, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amehamia katika afya baada ya kumsimamisha kazi daktari wa kitengo cha upasuaji katika Hospitali ya Ligula, Fortunatus Namahala kwa madai ya kumuomba mgonjwa rushwa ya Sh100,000.

Waziri Mkuu alichukua hatua hiyo jana alipotembelea hospitali hiyo ya mkoa na kukabiliwa na Tatu Abdallah ambaye alidai kwamba alilazimika kuuza shamba lake la ekari 2.5 ili apate Sh100,000 kwa ajili ya upasuaji wa baba yake.

“Februari Mosi nilimleta baba yangu hapa nikaambiwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji. Nikaandikiwa ninunue dawa za Sh85,000 hapo nje kwenye duka la dawa pia uzi wa kushonea kwa Sh25,000. Lakini pia daktari akasema anataka Sh100,000 ya kwake. Lakini hadi Februari 7 hakufanyiwa huo upasuaji,” alidai.



Pamoja na kutoa kiasi hicho cha fedha, Tatu alidai kuwa baba yake alitolewa wodini na kuambiwa arudi Februari 16. “Niliumia kwa sababu kijiji tunachotoka ni mbali na hali ya baba ilizidi kuzorota. Ndipo baba akaniambia nirudi kijijini kwetu Kilomba nikauze ekari 2.5 za shamba lake ili tulipie matibabu. Niliuza na kumpeleka baba katika Zahanati ya Sajora. Huko nililipa Sh560,000 na baba akafanyiwa upasuaji sasa hivi yuko nyumbani,” alidai.

“Leo nataka huyu daktari aje achukue boksi hili la dawa alizoniandikia na pia anirudishie hela yangu iliyopotea bure. Mie sijazitumia. Kwa nini aliniandikia wakati baba hajampa huduma yoyote?”

Alipoulizwa kama anaweza kumtambua daktari huyo akimuona, mama huyo alisema anaweza. Majibu ya mama huyo yalimfanya Waziri Mkuu kufanya gwaride la ukaguzi kwa kuwainua madaktari wote ili wajitambulishe na kumtaka mama huyo kumshika mkono mhusika.

“Gwaride la utambuzi ni jambo la kawaida. RPC hakikisha huyu mama hasumbuliwi. Lakini leo nitaanza na huyu daktari kwa sababu rushwa haivumiliki. RAS simamia suala lake lakini pia shirikiana na Takukuru na Polisi kufanya uchunguzi wa jambo hili hadi mwisho,” alisema.

Katika ziara yake hospitalini hapo, Waziri Mkuu pia alikutana na kero ya kukosekana kwa dirisha la dawa kwa wazee, daktari wa wazee na dirisha maalumu la wagonjwa wanaotumia bima ya afya.

Kadhalika, alielezwa kero za kuuziwa dawa kwa bei ya juu kwenye maduka ya dawa binafsi, lugha mbaya za madaktari na wauguzi, uchafu wa vyoo na uhaba wa maji.

Waziri Mkuu alitembelea wodi ya kinamama waliojifungua na kukuta wakiwa wametandikiwa shuka moja na wagonjwa kulazimika kuweka khanga juu ya mipira wanayolalia wodini ambayo walisema hutakiwa kujinunulia kabla ya kwenda hospitali kujifungua.

Akizungumza na watumishi wa hospitali hiyo, Waziri Mkuu alitumia muda mwingi kuwaeleza jinsi walivyo na umuhimu katika huduma zao. “Nafasi yenu ni nyeti kwa maisha ya binadamu hivyo mnapaswa kuwa na huruma na siyo kuwaumiza wananchi wa kipato cha chini ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu,” alisema.

Aliwataka waache tabia ya kuwatoza fedha watoto wanaolazwa hospitalini hapo na wanawake wanaojifungua kwani wanapaswa kutibiwa bure kwa mujibu wa sera ya Serikali.

Sakata la Hospitali ya Ligula lilianza Jumamosi iliyopita  wakati Waziri Mkuu akiwahutubia wakazi wa Mtwara kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mashujaa ambapo baadhi yao walipaza sauti kumtaka aende hospitalini hapo kwa kuwa kuna majipu ya kutumbua.

Waziri Mkuu aliwajibu kuwa amesikia ujumbe wao na kuahidi kufanya hivyo.

Kuhusu kero ya kuuziwa dawa kwa bei kubwa katika maduka binafsi, Waziri Majaliwa aliagiza kufungwa kwa maduka yote ya dawa yaliyo nje ya hospitali hiyo kuanzia leo na kumtaka Katibu Tawala wa Mkoa, Alfred Luanda kusimamia kazi hiyo hilo mara moja.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...