Thursday, December 25, 2014

UKAWA WATAKA SHERIA YA MAADILI INAYODHIBITI MAOVU

Viongozi wa Ukawa.

Viongozi wa UKAWA

VYAMA vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), vimetaka sheria ya maadili itungwe upya ili kuweka uwazi wa watu wote kuona taarifa ya mali za viongozi.

Vyama hivyo vinaamini hatua hiyo, itasaidia wananchi wote kujua mali halisi za viongozi na pia itasaidia kupunguza ufisadi, kutokana na wananchi kutambua ukweli wa mali za viongozi wao.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa umoja huo, Profesa Ibrahim Lipumba wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu hatua zinazostahili kuchukuliwa, kutokana na suala la uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Asante kwa kutembelea blog hii ya Jambo Tz, ili kuboresha blog yetu tunatoa fulsa ya kutangaza matangazo mbalimbali na pia kutoa maoni yako kupitia namba ya simu (WhatsApp & SMS) 0715 221198, E-mail jambotz8@gmail.com. Merry Chistmass & Happy New Year.
Alisema katika kikao kijacho, Bunge linatakiwa kufikiria kuiwajibisha Serikali kwa kutotekeleza kikamilifu maazimio yake. “Vyama vya siasa vya Ukawa kwa kushirikiana na wabunge, vitaendelea kuelimisha umma kuhusu ufisadi wa akaunti ya Tegeta Escrow, ili wananchi waelewe juu ya ufisadi huu,” alisema Lipumba.
Aidha, alisema umoja huo utaitisha maandamano nchi nzima ya kuulani kile kinachoitwa ufisadi wa Escrow na kushinikiza utekelezaji wa maazimio ya Bunge, iwapo maazimio yote yaliyopendekezwa hayatatelezwa.
Alisema hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote waliosababisha ufisadi huo na walionufaika na fedha hizo. Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema umoja huo unahitaji kuwa na taifa lenye umoja kwa sababu Tanzania ni ya wananchi wote na hakuna mwenye hatimiliki ya Tanzania.
“Yale maazimio nane ya Bunge ni wananchi, Bunge ni chombo cha wananchi na ni mazimio ya maridhiano ya kuliweka taifa pamoja,” alisema Mbatia.
Alisema maandamano hayo yatakayofanyika, yatakuwa na lengo la kuwaeleza Watanzania ukweli na si vinginevyo. Lakini wakati hao wakifikiria kufanya hayo, Rais Kikwete, wakati akilihutubia taifa kupitia wazee wa mkoani wa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, alitoa majibu ya maazimio yote nane ya Bunge, ikiwa pamoja na kumwajibisha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi amesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili, huku Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akiwekwa kiporo.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema naye amejiuzulu, akisema ushauri wake katika sakata la Escrow haukueleweka, ingawa anasisitiza hakuona kosa lolote.
Akitolea maamuzi ya maazimio mengine, akianzia na lile linalotaka Serikali iangalie uwezekano wa kuchukua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO kwa mujibu wa Sheria za nchi, Rais Kikwete alisema ni jambo linalowezekana.
Hata hivyo, alitaka busara itumike kwa kuwa uamuzi huo unaweza kupeleka ujumbe mbaya kwa wawekezaji, na hivyo kuwakatisha tamaa ya kuwekeza nchini.
Kuhusu azimio la uwazi wa mikataba, alisema ni wazo zuri, hivyo serikali na Bunge watakaa kutafuta namna bora ya kisheria katika mikataba.
Azimio jingine limetaka Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama, vichukue hatua stahili kwa mujibu wa sheria za nchi yetu dhidi ya watu waliotajwa kwenye taarifa maalum ya Kamati husika na vitendo vyote vya kijinai kuhusu miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea kuhusu kuhusika kwao katika vitendo hivyo vya jinai.
Akijibu kuhusu azimio hilo, Rais Kikwete alisema: “ Vyombo husika vimekwishaagizwa kufanya hivyo na kazi imeanza na inaendelea. Ikiwa wapo watu wenye makosa hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.”
Alijibu pia azimio la kutaka wenyeviti wa Kamati za Bunge waliotajwa katika sakata la Escrow wavuliwe nyadhifa, alisema hilo liko chini ya mamlaka ya Bunge lenyewe, hivyo ameachia waamue.
Kuhusu uundwaji wa Tume ya Kijaji ili kuchunguza utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania, alisema amelipokea, lakini suala hilo linapaswa kuanzia kwenye mhimili wa Mahakama yenyewe na siyo kwa Rais au Bunge, hivyo Jaji Mkuu ndiye anayepaswa kulishughulikia.
Rais Kikwete pia alitoa maelezo na maamuzi mengine kuhusu maazimio ya Bunge, aliyosisitiza anayeheshimu, hivyo kwa ujumla kuonekana kukonga nyoyo za wengi waliokuwa wanasubiri kusikia kauli na maamuzi yake juu ya sakata la Escrow, lililoibua mjadala mzito wakati wa Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge, ulioketi kwa mwezi mmoja hadi Novemba 28 mwaka huu.
Asante kwa kutembelea blog hii ya Jambo Tz, ili kuboresha blog yetu tunatoa fulsa ya kutangaza matangazo mbalimbali na pia kutoa maoni yako kupitia namba ya simu (WhatsApp & SMS) 0715 221198, E-mail jambotz8@gmail.com. Merry Chistmass & Happy New Year.

Na Habari Leo 

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...