Rais Jakaya Kikwete
anatarajiwa kuwasili Dodoma keshokutwa, ikiwa ni siku moja kabla ya
kuwasilishwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15.
Habari zilizopatikana jana zinasema
Rais ataongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kitakachopewa muhtasari
kuhusu Bajeti ya Serikali ya mwaka ujao wa fedha na baadaye atafuatilia
uwasilishaji wa bajeti hiyo bungeni akiwa Dodoma.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva
Rweyemamu alisema asingeweza kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yuko
likizo lakini akaweka bayana kwamba kwa kawaida kabla ya bajeti
kuwasilishwa bungeni, lazima Baraza la Mawaziri lipewe muhtasari wa
bajeti husika.
"Ni kawaida kabla ya bajeti
kuwasilishwa, Rais huongoza kikao cha Baraza la Mawaziri yaani pre
budget cabinet meeting ambako Waziri wa Fedha hutoa briefing (muhtasari)
kuhusu maeneo muhimu ya bajeti, kwa hiyo siyo jambo jipya ni suala la
kawaida," alisema Rweyemamu.
Itakumbukwa kuwa mwaka jana kabla ya
kusomwa kwa bajeti ya 2013/14, Rais Kikwete alikuwa Dodoma ambako pamoja
na kukutana na mawaziri, pia alifanya kikao na Kamati ya Bunge ya
Bajeti.
Hata hivyo, uwepo wake mjini Dodoma
safari hii umekuja wakati kukiwa na dalili za mvutano mkubwa kati ya
Bunge na Serikali kutokana na kutotolewa kwa fedha za kutosha za
maendeleo kwa mwaka wa fedha unaoisha Juni 30 mwaka huu. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz