Askari na wakazi wa Buguruni Malapa, Dar es Salaam wakitazama nyumba iliyoteketea kwa moto na kuua watu tisa wa familia moja usiku wa kuamkia jana.
Watu tisa wa familia moja wameteketea kwa moto baada ya nyumba yao kuungua usiku wa kuamkia jana jijini Dar es Salaam, huku mashuhuda wakisema walikuta miili yao ikiwa imeshikana.
Juhudi za kuwaokoa watu hao waliofariki dunia wakiwa kwenye moja ya vyumba vya nyumba hiyo namba 40 iliyoko katika Mtaa wa Ulam, Buguruni Malapa wilayani Ilala, zilishindikana na chanzo cha moto huo hakijajulikana ingawa mashuhuda wanasema mtungi wa gesi ulilipuka baada ya moto kuwaka kwa muda mrefu.
Walioteketea katika tukio hilo ni mama wa familia hiyo, Samira Juma Ibrahim (42), maarufu kwa jina la Mama Aisha na watoto wake wanne, Ahmed Masoud (15) aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Aisha Masoud (17), aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la sita, Abdillah Masoud (10) na Ashraf Masoud (5).
Wengine ni Bimdogo Masoud (72), ambaye alikuwa mgonjwa na mama wa Samira, pamoja na wadogo zake wawili wa kike, Samira Harood (17) na Wahat Saleh (27), ambaye alitokea Unguja, pamoja na Fahir Fesal mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page yetu ya facebook bofya Jambo Tz sasa.