Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
Taifa, Rais Jakaya Kikwete amewataka wanachama wa chama hicho kuacha
unyonge na kusema uvumilivu una kikomo chake.
Aliyasema hayo jana wakati anafungua
kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, kilicholenga kuweka
msimamo wa chama kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya ambayo inaanza kujadiliwa
Jumanne wiki ijayo.
"Tuna uchaguzi mdogo, Iringa, Kalenga,
tumeshapata mgombea na tumefanya hiyo kazi kwa niaba yenu kwa sababu
hatukupata muda wa kuitisha Kikao cha Halmashauri Kuu, lakini mmetupatia
mamlaka ya kufanya hivyo na Katiba imetupa fursa ya kufanya uteuzi kwa
niaba yenu,"alisema.
CCM imemteua Godfrey Mgimwa ambaye ni
mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, marehemu Dk William Mgimwa,
kupeperusha bendera katika uchaguzi mdogo utakaofanyika baadaye mwaka
huu. Dk Mgimwa hadi anafariki dunia alikuwa Waziri wa Fedha.
Uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la
Kalenga lililopo mkoani Iringa unatarajiwa kufanyika Machi 16, mwaka
huu, huku tayari vyama vya CCM na Chadema vikiwa vimetaja wagombea wake,
Chadema kikiwa kimetangaza, Grace Tendega Mvanda.
Rais Kikwete alisema chama hicho kinashindana na vyama vingine katika uchaguzi huo mdogo.
"Tunashindana na wenzetu wagomvi,
maana wao ugomvi ndiyo sehemu ya mwongozo wa kufanya kazi ya
siasa,"alisema Kikwete bila kutaja chama chochote cha siasa kwa jina.
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz