Sunday, February 16, 2014

UMECHOKA KUAJIRIWA UNATAKA KUJIAJIRI?! HAYA HAPA MAMBO 8 MUHIMU YA KUZINGATIA


Kuna sababu mbalimbali kwanini mtu atake kuajiri, badala ya kuajiriwa, mfano kipato kidogo anachopata katika kazi husika, hitaji la kutaka uhuru zaidi binafsi wa kufanya kazi, hitaji la kuweza kutoa ajira kwa wengine na zaidi sana kuweza kutumia vema kipaji na uwezo wa kuzalisha ambao katika kazi ya sasa mtu hapati nafasi ya kufanya hivyo.  
Kujiajiri ni jambo linalohitaji maandalizi ya muda mrefu na kuna mambo ya msingi kuyafahamu, haiwezekani tuu , ukaacha kazi na kusema ok, acha nijiajiri.
Makala hii inachambua mambo ya msingi ya kujiandaa na kuyafahamu kabla mtu hajaamua kuacha kuajiriwa.
 
Mkakati ni muhimu: Wazo au ndoto isiyo na mkakati wa kuitimiza ni upuuzi yaani ndoto hiyo au wazo hilo halina maana, hivyo basi ndoto yako ya kujiajiri siku moja, ni lazima iwekewe mkakati wa kuifanikisha ikiwa ni pamoja na muda hasa wa lini utaitimiza hiyo ndoto. 
Katika kuweka mkakati huu wa kutimiza ndoto yako, fanya utafiti wa kina kuhusu mipango yako binafsi ya maisha, mtazamo wako kuhusu maisha, mpenzi/mke wako, familia yako, na hali ya jamii kwa ujumla inavyoenda kama vile mabadiliko ya hali ya kisiasa, teknolojia, na uchumi. 
Tengeneza malengo ya aina ya shughuli unayotaka kuifanya ukiacha kuajiriwa, na pima uwezekano wa shughuli hiyo kufanyika kweli na kama itakulipa. Utambue pia aina ya watu na rasilimali nyingine utakazozihitaji, na jinsi utakavyozipata. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz
Unahitaji fedha: Ndio, unahitaji kiasi cha fedha za kutosha kununua vifaa na malighafi za kutengenezea bidhaa yako. Pia unahitaji fedha za kuwalipa wafanyakazi wako, na zaidi sana , unahitaji fedha za kuendesha maisha yako na familia yako , kwa kipindi fulani kabla ya biashara kuanza kukulipa mshahara. Hivyo kabla haujaacha kibarua chako, hakikisha umetengeneza bajeti ya kutosha na una akiba ya kutimiza mahitaji ya bajeti yako. Usingependa uache kazi halafu uanze kuwa omba omba kwa rafiki na jamaa, au uanze kujuta.

Network ni muhimu: Kumbuka katika kujiajiri kwako, utahitaji wateja, washirika, wafanyakazi na hata washauri mbalimbali ili mambo yako yaende vizuri. Hivyo, wakati ukiwa umeajiriwa ndio wakati wako muafaka wa kutengeneza na kupanua wigo wako wa watu unaowafahamu na waliokaribu nawe.
Kumbuka kuendeleza mawasiliano kwani watu hawapendi kuona wewe unataka kuwatumia tuu kisha unawatupa. Endeleza mawasiliano walau hata kwa salamu tuu. Zaidi sana, heshimu watu wote, hata usiowafahamu au wale unaodhani 'sio watu muhimu'. 
Jenga taswira nzuri kwa jamii kwa lugha fasaha, picha na matukio mengine, usifanye watu wakufikirie vibaya.

Usipitwe na wakati: Hakikisha kuwa unafuatilia taarifa za matukio, dili na watu wanaohusiana na aina ya shughuli unayopanga kuifanya wakati utakapojiajiri. Hii itakusaidia kupata uzoefu na kusoma alama za nyakati, na pengine kutambua fursa nyingine zaidi. 
Endelea kujifunza zaidi kuhusu kazi yako, watu na jamii kwa ujumla kwani kujiajiri kunahitaji uzoefu zaidi, na zaidi sana uwezo wa kupambana na changamoto nyingi ambazo nyingine haujawahi kukutana nazo kabisa, ila taarifa za awali na kujua jinsi mambo yanavyoenda kwa ujumla katika jamii vitakufanya ushinde changamoto.

Maana halisi ya biashara: Baada ya kuacha kuajiriwa, hautarajii kuwa mtu wa ‘kuganga njaa’ yaani kufanya biashara ili mradi tuu hela iingie, lakini haujui mwelekeo wa biashara yako upoje, na wala hakuna mkakati wa kuikuza na kuimarisha biashara husika. 
Biashara inahusu kutimiza mahitaji ya watu, kwahiyo ili mradi utakuwa na uwezo mkubwa wa kutimiza mahitaji ya watu, na kuendelea kuhamasisha watu zaidi kuja kwako uweze kutimiza mahitaji yao , basi biashara itakua, na itaendelea kuwa endelevu. 
Kinyume cha hapo, ushindani utakutoa katika biashara kwani wateja watakambilia kwa wengine. Biashara sio tuu kupata wateja, ni vile kuweza kuendelea kupata wateja na kuendelea kupanua biashara. 
Inabidi uipende shughuli husika unayoifanya, na uweze kutimiza mahitaji ya wateja kupitia biashara husika. 
Muda wako mwingi utautumia katika shughuli yako mpya utakayojiajiri hivyo, kama ambavyo kazi uliyonayo pengine ‘inakuboa’, hakikisha ajira yako binafsi ‘haikuboi’.

Umuhimu wa wafanyakazi: Watendaji wa shughuli husika za biashara yako utakayoianzisha ni muhimu wawe wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha wa kufanya shughuli husika, na uweke mikakati ya kuwapatia nyenzo zote muhimu za kufanyia kazi ikiwemo teknolojia na mazingira mazuri ya kazi. Hivyo basi wakati unajiandaa kujiajiri tilia maanani hili katika bajeti yako ya kuajiri. Usingependa wafanyakazi wao wajisikie vibaya kama vile wewe ulivyojisikia vibaya katika ajira yako fulani (pengine ajira yako ya sasa). Muda huu ambao umeajiriwa, ndio muda pia muafaka wa kusaka 'vipaji'- yaani watu ambao utafanya nao kazi utakapojiajiri. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz

Inakuhusu wewe : Mafanikio yako katika kujiajiri yanategemea mambo mengi ila zaidi sana yanakutegemea wewe. Je, nini hasa sababu yako ya kutaka kujiajiri? 
Ni kweli una bidhaa au huduma haswa ya kupeleka sokoni itakayokufanya iendeshe maisha yako na kuiendeleza biashara husika au ni hasira tuu za jinsi bosi wako anavyokuchulia hapo ofisini kwako, au kwakuwa mshahara uliopo sasa haukutoshi. Je, mipango yako mingine ya maisha ipoje? 
Ndoto zako za kusoma, au kuishi sehemu tofauti tofauti, pengine mkoa mwingine tofauti na uliopo sasa, au pengine hata nchi husika. Je, yote hayo yanaathiri vipi mipango na mikakati yako ya kujiajiri, bila kusahau msukumo toka kwa familia yako.

Ndoto sahihi: Ni kweli kuwa upo sahihi kufikiria au kuota kufanya biashara kubwa na yenye mafanikio sana, lakini kumbuka mafanikio hayaji kwa usiku mmoja, na hata kama yatakuja kwa usiku mmoja, inahitajika kazi ya muda mrefu kuyafanya yawe endelevu. 
Hivyo basi, usingoje wakati ‘muafaka’ wa wewe kuwa na kiasi kikubwa cha fedha au kwamba ‘umeyaset’ vema mambo yote. 
Anza kidogo kidogo, kubali kufanya makosa, na tambua kuwa hata kama utafanya uchambuzi na uchunguzi wa kutosha kuhusu soko, jamii na teknolojia, hali halisi unayoenda kukumbana nayo inaweza kuwa tofauti na ile uliyojifunza wakati wa uchambuzi au uchunguzi wako kwakuwa hicho unachoenda kufanya ni kipya hakikufanyiwa uchambuzi, bali unakifanya kutokana na uchambuzi uliofanya hapo awali. 
Kuna mtu mwingine atakuja kutumia makosa au mafanikio yako kupanga mambo yake. 
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz.
Na Mbuke

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...