MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Chalinze Mzee, wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, Elias Kapama, yuko katika wakati mgumu baada ya kuhamishia ofisi yake kwenye vyoo vya wanafunzi kutokana na jengo la ofisi yake kuharibika vibaya.
Hatua ya kuhamia chooni ilitokana na mkuu huyo kutawaliwa na hofu ya ubovu wa ofisi yake, hivyo kushindwa kufanya kazi zake kwa ufasaha unapotokea upepo au mvua.
Novemba 2012, Kapama alihamishia ofisi yake katika jengo la vyoo vya wanafunzi ambavyo havijaanza kutumika tangu ujenzi wake ukamilike mwaka 2011. Akizungumzia hali hiyo, Kapama alisema kuwa anajisikia vibaya kutumia chumba maalumu cha kubadilishia nguo cha wavulana katika choo hicho kutokana na kukosa msaada kutoka halmashauri ya wilaya hiyo.