The Finest : FA apata wakati mgumu kwa kulazimishwa na mashabiki kutaja jina la Lady Jay Dee.
Mwanamuziki
Hamis Mwinjuma, maarufu Mwana FA, amepata wakati mgumu kwa
kulazimishwa na mashabiki kutaja jina la Lady Jay Dee, baada ya
kuliruka jina hilo alipokuwa akiimba wimbo wa Mabinti ambao ndani yake
kuna jina la Jay Dee.
Mwana FA alisita kwa muda na baadaye aliamua kurudia wimbo huo na alipofika katika kipengele cha kumtaja Jide aliimba kwa kumtaja, hali iliyoufanya ukumbi huo ulipuke kwa shangwe na mashabiki kumtaka arudie tena na tena.
Kutokana na hilo FA aliamua kufunguka; “Tunaishi na watu hivyo lazima mtagongana, hata mapacha wanakosana na kusameheana, lakini wakati mwingine shida inawafanya mnapatana,” alisema Mwana FA.
Awali
shoo ilitangazwa kuwa ingekuwa ya watu 400 tu. Lakini mpaka inafika
saa nne kasoro usiku, muda uliotangazwa kuanzwa kwa shoo hiyo watu
waliokuwa wamefika walikuwa kama 250 tu.
Saa
nne kamili mwanamuziki Hamis Mwinjuma, Mwana FA alikanyaga ‘red
carpet’ akiwa na mbunifu wa mavazi Sheria Ngowi, na baada ya
kuchukuliwa picha kadhaa alianza kuelekea nje ya ukumbi sehemu
waliyosimama watu wakipata chakula na vinywaji, watu walizidi kufurika
lakini kila aliyeingia alikuwa alwatan kidogo.
Waliendelea kuwasili mastaa na shoo inaanza Mashabiki wanaanza kuingia ukumbini saa tano kamili baada ya kupata vyakula na vinywaji nje, huku muziki wa taratibu ukipigwa na bendi ya muziki wa dansi ya Njenje. Mashabiki wanaendelea kubadilishana mawazo mpaka inapotimu saa tano na robo usiku, ambapo Mwana FA anapanda jukwaani.
Anaanza kazi kwa shoo ya aina yake baada ya kuimba hip hop live akiwa na bendi ya muziki wa dansi, kwenye shoo hiyo iliyofanyika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam.
FA
alipanda jukwaani na wimbo wa Binamu akisindikizwa na wanamuziki
Mandojo na Domokaya waliovalia suruali nyeusi na mashati meupe huku
wakiwa wamevalia mikanda aina ya ‘suspender’, baadaye aliimba wimbo
Unanijua Unaniskia na Bado Niponipo Kwanza ambao uliwapendeza
mashabiki.
Alisimamisha shoo kwa muda na msanii Bernald Paul maarufu kama Benpol alipanda jukwaani na kuimba nyimbo zake tatu kwa kuziunganisha ukiwamo wa Maneno, Pete na Nikikupata na baadaye aliimba na Mwana FA wimbo wa Asubuhi aliomshirikisha Q Chief.
FA alipanda jukwaani na wanamuziki kadhaa katika vipindi tofauti akiwamo Linah Sanga ‘Linah’, Maua, Abdul Sykes ‘Dully Sykes’.
Baadhi
ya nyimbo alizoimba ni pamoja na Kama Zamani, Alikufa kwa Ngoma,
Habari Ndio Hiyo, Leo, Mabinti, Unanitega, Yalaiti na nyingine nyingi.