JEURI ya pesa. Ndicho unachoweza
kusema baada ya klabu tajiri Ulaya, Paris Saint-Germain na Manchester
City kudaiwa kuwa zipo tayari kumng'oa, Lionel Messi, kutoka Barcelona
kwa gharama yoyote ile.
Wakati ikiwekwa wazi kwamba thamani ya
supastaa huyo wa Kiargentina ni Euro 400 milioni, klabu hizo
zinazomilikiwa na matajiri wenye pesa ndefu, zimesema zipo tayari.
Ripoti zinabainisha kwamba uamuzi wa
kumfanyia tathmini Messi ili kufahamu thamani yake halisi, umefanywa
mahususi na klabu hizo ili kufahamu itawagharimu kiasi gani ili kuipata
saini yake. Kwa mtazamo wa kawaida anaonekana mchezaji huyo ni kama
hanunuliki.
Kwa mujibu wa tathmini hiyo
iliyofanywa na klabu tatu za Ulaya zenye pesa za kutosha, staa huyo wa
Barcelona na mshindi mara nne wa Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia (Ballon
d'Or), thamani yake ya sasa inazidi kipengele kilichowekwa kwenye
mkataba wake kwamba anaweza kuuzwa kwa Euro 250 milioni.
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz