Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WASHAMBULIAJI wa kimataifa wa
Tanzania, Mbwana Ally Samata na Thomas Emmanuel Ulimwengu kesho jumapili
wanatarajia kuiongoza TP Mazembe katika mchezo wa hatua ya makundi ya
ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya wapinzani wao wakubwa, AS Vita
mjini Lubumbashi.
Timu hizi hasimu zitakutana
katika mchezo wa kesho zikiwa na kumbukumbu ya kusababisha maafa ya vifo
vya watu zaidi ya 15 katika mchezo wao wa ligi kuu ya DR Congo wiki za
karibuni.
Tukio hilo baya lilitokea mjini
Kinshasa baada ya mashabiki wa AS Vita kutoridhishwa na kipigo cha bao
1-0 kutoka kwa wapinzania wao TP Mazembe.
Mchezo wa kesho umevuta hisia za
mashabiki wengi wa soka, kwani timu hizi zinapokutana, upinzani
unakuwabmkubwa mno nje ya uwanja na ndani ya uwanja.
TP Mazembe wataingia katika
mchezo wa kesho wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kupigwa bao 1-0 kwenye
mchezo wao wa kwanza wa kundi A na Al Hilal ya Sudan mnao mei 17 mwaka
huu.
Mei 18 mwaka huu, AS Vita
walitumia vyema uwanja wao wa nyumbani baada ya kuilaza Zamalek ya Misri
mabao 2-1, hivyo wataingia katika mchezo huo wa kundi A wakiwa na
morali kubwa ya kusaka ushindi wa pili.
Mechi nyingine ya kesho jumapili itakuwa ya Kundi B kati ya wenyeji ES Setif ya Algeria dhidi ya SC Sfaxine ya Tunia.
Mei 18 mwaka huu SC Sfaxine
waliifumua Al Ahly Benghazi ya Libya mabao 3-1, wakati mei 17, 2014, ES
Setif waliifunga mabao 2-1 Esperance ya Tunisia.
Mbali na mechi hizo za kesho, leo
hii mitanange mingine inaendelea ambapo kundi A, wenyeji Zamalek
watawakaribisha Al Hilal kutoka nchini Sudan.
Huu utakuwa mchezo muhimu kwa
Mafarao waliopoteza mechi iliyopita. Al Hilal wao watakuwa wanahitaji
ushindi wa pili katika michuano hiyo.
Mechi ya kundi B leo hii, wenyeji
Al Ahly Benghazi ya Libya waliopoteza mechi ya kwanza kwa mabao 3-1
watakabiliana na miamba ya soka la Tunisia, Esperance ambao nao mechi ya
kwanza walilala kwa mabao 2-1. Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz