Dodoma/Dar es Salaam. Ni
matukio nadra kutokea katika maisha, lakini haya ndiyo yaliyomkuta
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Vicky Kamata, baada ya kuugua ghafla saa
36 kabla ya harusi yake.
Kuugua kwa bibi harusi huyo mtarajiwa, kumezua
gumzo katika Viwanja vya Bunge mjini Dodoma na maeneo mengine nchini,
kutokana na kile kilichoelezwa kwamba harusi hiyo ilipangwa kuwa ya
kifahari ikitarajiwa kutumia Sh96 milioni.
Kamata ilikuwa afunge ndoa leo katika Kanisa
Katoliki Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mkombozi, Sinza Dar es Salaam
na tayari kadi za mialiko zilishasambazwa kwa watu mbalimbali wakiwamo
wabunge.
Habari za kuugua ghafla kwa mbunge huyo ambaye pia
ni msanii wa muziki aliyetamba na kibao chake cha ‘Wanawake na
Maendeleo’ zilianza kuzagaa kwa kasi juzi jioni nchini. Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz
Kamata ambaye pia ni mtetezi wa haki za
wanawake, aliugua usiku wa kuamkia jana na kupelekwa katika Hospitali
ya Tabata General, iliyopo Segerea ambapo amelazwa. “Niliugua tumbo ghafla, nilipata maumivu makali
sana nikampigia daktari wangu na nilipomweleza jinsi ninavyojisikia,
aliniambia niende hospitali haraka na kutokana na hali ilivyo, waliamua
nilazwe,” alisema Kamata akiwa kitandani katika hospitali hiyo.
Kamata alifafanua kuwa, pamoja na mambo mengine,
hali yake ya ujauzito imekuwa ikimsumbua na kuchangia yeye kulazwa kwa
mara ya pili sasa katika kipindi cha wiki mbili. Mbunge huyo ambaye
alitakiwa kufunga ndoa leo, alisema kuwa kutokana na maradhi hayo,
haelewi hatima ya ndoa yake, ingawa wanafamilia na wanakamati
wanaendelea na mipango ya harusi kama ilivyopangwa.
“Mama anaenda nyumbani sasa hivi kuniandalia nguo
na kila kitu, lakini sijui itakuwaje kwa sababu daktari amesema kutokana
na hali yangu ilivyo, itakuwa vigumu kuvaa viatu virefu na kupata
usumbufu wote wa purukushani za harusi,” alisema.
Aliongeza kuwa mipango yote ya harusi ipo tayari
kinachosubiriwa na siku yenyewe, lakini kwa bahati mbaya jambo hilo
limetokea na haliwezi kuepukika. Vicky alisema wanakamati wa Dar es Salaam na wale
wa Dodoma, wanaendelea na vikao ingawa, wamechanganyikiwa kutokana na
sintofahamu iliyopo, kama harusi itafanyika au haitafanyika.
Ndugu wa mbunge huyo akiwemo mama yake mzazi
Kamata walionekana hospitalini hapo wakiendelea kumfariji na kujadili
kuhusu hatima ya harusi hiyo, iliyokuwa ikingojewa kwa hamu na
wanafamilia wote.
Daktari wa Kamata, aliyefahamika kwa jina la
Diwani Msemo, alieleza kuwa mbunge huyo alifika hospitalini hapo akiwa
na maumivu makali ya tumbo yaliyofanana na uchungu wa kuzaa, hali
iliyoonyesha kuwa ujauzito wake unatishia kutoka.
“Ukipata yale maumivu kama mimba ni changa inakuwa kama tishio
la mimba kutoka, siyo hivyo tu, bali alikuwa anatapika na presha
ikashuka. Kwa kweli mimba yake ipo katika hatari,” alisema
Alisema pamoja na kumpa matibabu, walishauriana
kuwa apumzike kwa siku tano ili kuhakikisha kiumbe kilichopo tumboni
kipo salama. Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz
“Ilikuwa ni uamuzi mgumu kwa sababu ni siku yake
ya harusi, lakini tunaangalia umuhimu wa kiumbe na kama ataenda, itabidi
asaini ili ijulikane kuwa hatukumkubalia. Kwa kifupi hayuko fiti kwa
shughuli hiyo,” alisema. Harusi ya Kamata iliandikwa pia na mitandao
mbalimbali ya kijamii nchini na jana redio moja ilitangaza kuugua kwake,
ikisema kumetokana na matatizo ya ujauzito. Kumekuwa na uvumi unaosambazwa kwa kasi juu ya
sababu za kuahirishwa kwa harusi hiyo, lakini kwa sababu ya maadili ya
uandishi hatutaweza kuziandika katika gazeti hili.
Paroko aliyekuwa afungishe ndoa anena
Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria
Mama wa Mkombozi , Sinza Dar es Salaam, Cuthbert Maganga alipohojiwa
kuhusu taarifa za kufungwa kwa ndoa hiyo, alikiri kwamba iliandikishwa
ili ifungwe kanisani hapo. Hata hivyo akasema ilishindikana, baada ya
wahusika kukwama kuwasilisha baadhi ya nyaraka muhimu zilizohitajika,
ili kukamilisha sakramenti hiyo.
“Ilitarajiwa kufungwa Mei 24 mwaka huu yaani
kesho (leo), lakini kwa taratibu za kanisa letu ilishindikana kwa sababu
bibi harusi alishindwa kuwasilisha cheti chake cha ubatizo, pia hakuwa
amepata kipaimara, vitu hivyo ni miongoni mwa vitu muhimu
vinavyohitajika ili kukamilisha Sakramenti ya Ndoa,” alisema Padri
Maganga.
Alisema Kamata ndiye aliyekwenda kuandikisha ndoa hiyo, kwa kuwa ni muumini wa kanisa hilo anayetokea Kanda D. Juhudi za kumtafuta bwana harusi, Charles Gardner
hazikuweza kufanikiwa baada ya simu yake kuita bila kupokelewa, hata
alipotumiwa ujumbe wa maandishi hakuwa tayari kujibu.
Hata hivyo, baadhi ya rafiki wa karibu wa Gardner
walieleza kuwa wamejulishwa kuwa ndoa hiyo haipo na kwamba jana bwana
harusi huyo mtarajiwa alionekana akiwa katika hali isiyo ya kawaida.
“Nilijaribu kumuuliza kuhusu harusi yake, lakini hakuwa tayari
kunieleza bayana, ila hayupo katika hali yake ya kawaida,” alisema mmoja
wa rafiki zake. Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz
Imeandikwa na Florence Majani, Daniel Mjema na Beatrice Moses
No comments:
Post a Comment