Baada
ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kutoa mwongozo na kuunga mkono uamuzi
wa Naibu wake, Job Ndugai kuwasimamisha wabunge sita wa Chadema, wasomi,
wanasiasa na wanaharakati wamesema Kiti cha Spika ndiyo chanzo cha
mvutano bungeni kwa kuwa kinapendelea wabunge wa chama tawala (CCM).
Wamesema
licha ya Bunge kuongozwa na kanuni, wakati mwingine viongozi hao wa
Bunge wanatumia kanuni hizo kuwapendelea wabunge wa CCM, huku wakieleza
kuwa licha ya wabunge wa chama hicho kutukana, hawakupewa adhabu yoyote.
Jumatano
ya wiki hii, Ndugai aliwasimamisha Tundu Lissu (Singida Mashariki),
Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini),
Highness Kiwia (Ilemela), Ezekiah Wenje (Nyamagana) na Godbless Lema wa
Arusha Mjini kutohudhuria Bunge kwa siku tano kutokana na alichokiita
kufanya vurugu ndani ya Bunge.
Uamuzi
huo wa Spika Makinda ulikuja baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kumtaka Ndugai aeleze alitumia kanuni
gani kuwasimamisha wabunge hao.