Maandalizi
ya msimu wa ligi kuu ya Tanzania yameanza kupamba moto huku vilabu
vikijaribu kujiimarisha tayari kwa mapambano, kwa upande wa klabu ya
Yanga wameanza kwa kuimarisha benchi la ufundi kwa kumuajiri kocha
Marcio Maximo.
Kocha huyo mbrazil anayeheshimika zaidi nchini, Marcio Maximo atatua
Jangwani ndani ya siku nne kuanzia leo Jumamosi. Bosi huyo ambaye
anasifika zaidi kwa msisitizo wake katika nidhamu za wachezaji atatua
Jumanne ikiwa ni mapema kabla ya uchaguzi wa Simba utakaofanyika Juni 29
Jijini Dar es Salaam. Mwanaspoti linajua kwamba Maximo yuko jijini
Brasilia akifanya kazi ya uchambuzi wa mechi za Kombe la Dunia kwenye
televisheni ya Taifa ya Mexico na mkataba wake unamalizika Jumatatu.
Yanga imethibitisha kwamba Maximo ameshaanza maandalizi ya safari
hiyo tangu juzi ambapo katika hilo pia amewajulisha baadhi ya maofisa wa
Ubalozi wa nchi hiyo nchini kuwa atakuwa Tanzania mapema wiki hii
kumalizia maongezi yake na mabosi wa Yanga.
Yanga wamemleta Maximo mapema kufanya maandalizi ya uhakika katika
kikosi cha timu hiyo ikiwa ni kuwawahi wapinzani wao wa jadi Simba ambao
bado wapo katika mchakato wa uchaguzi.
“Ilikuwa kuna baadhi ya viongozi waende Brazil kumalizia mazungumzo
na kusainishana mkataba lakini hilo limebadilishwa. Maximo ndiyo
atakuja Dar es Salaam kuepuka gharama,”alisisitiza mmoja wa viongozi wa
Yanga.
Source: Mwanaspoti