Rais wa Marekani Barack Obama ametoa pongezi na sifa kwa Tanzania kwa
kuwa miongoni mwa nchi chache duniani ambazo zimetia saini mkataba wa
Ushirikiano wa Serikali Zinazoendeshwa kwa Uwazi ambao unalenga kujenga
na kuendeleza nafasi ya taasisi zisizokuwa za Kiserikali katika utawala
bora, uwazi na uwajibikaji katika uendeshaji wa Serikali.
Rais Obama ametoa pongezi hizo kwa Tanzania leo, Jumatatu, Septemba 23,
2013, wakati akizungumza katika mkutano maalum aliouandaa mwenyewe Rais
Obama kuzungumzia nafasi za Serikali katika kuunga mkono na kuendeleza
asasi na taasisi zisizokuwa za Kiserikali na kuzishirikisha zaidi katika
kuboresha shughuli za utawala bora uliofanyika kwenye Hoteli ya Hilton,
mjini New York, Marekani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi wachache duniani walioalikwa
kushiriki mkutano huo maalum ambao pia ulishirikisha wawakilishi wa
asasi zisizokuwa za Kiserikali 300.
Baadhi ya nchi nyingine za Afrika zilizoalikwa na kushiriki katika
mkutano huo ni pamoja na Liberia, Ghana, Benin, Libya, Tunisia, Senegal,
Afrika Kusini na Botswana.
Shabaha kuu ya mkutano huo wa saa moja ilikuwa ni kutafuta namna ya
kuongeza kiwango cha kuungwa mkono kwa taasisi na asasi hizo na jinsi
gani ya kuzilinda ili kuziwezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Aidha, mkutano huo ulilenga kuzitaka Serikali ambazo zinaweka vikwazo
kwenye utendaji wa asasi hizo kuondoa vikwazo hivyo haraka ambavyo
vinahujumu utendaji kazi na mchango wa asasi hizo katika uendeshaji wa
utawala bora.