Na Dina Ismail
KAMATI ya utendaji ya klabu ya Simba inatarajiwa kutoa uamuzi mgumu
kuhusiana na mwenendo mbaya ulionayo timu hiyo katika ligi kuu ya
Vodacom.
Aidha, Rage amekanusha taarifa za kujiuzulu kwake kufuatia mwenendo mbaya wa timu hiyo kwenye ligi hiyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, mwenyekiti wa Simba Alhaj Ismail
Aden Rage alisema kwamba kamati ya utendaji ya Simba ilitarajiwa
kukutana jana kwa ajili ya kujadili mustakabali wa timu yao.
Alisema kikao hicho kitajadili kwa kina hali iliyopo sasa ambayo
imesabababisha timu yao kupoteza hata matumaini ya kutetea ubingwa wao.
“Tutakuna baadaye leo na kujadili hali hii maana tukiiacha hivi hivi
inaweza kutuletea madhara makubwa sana…pia tutatoa maamuzi mazito baada
ya kikao chetu,”alisema.
Kuhusu na taarifa za kujiuzulu kwake, Rage alisema anashangazwa na
taarifa hizo zinapotoka kwani kama atafikia uamuzi huo ataitisha mkutano
na waandishi wa habari na kuzungumzia hatua hiyo.
“Mimi sijasema nitajiuzulu jamani hata hiyo taarifa yenyewe ukiisoma
haileweki, hivyo nawaomba wanasimba kutulia kuona kipi
kitakachofuata,”aliongeza Rage
Simba imeonekana kusuasua sua katika ligi hiyo baada ya kutokuwa na
matokeo ya kuridhisha sambamba na kuamulia vipigo katika mechi zake.
Hali hiyo ilianza kujitokeza tangu mwishoni mwa mzunguko wa kwanza wa
ligi hiyo ambao ulipelekea kutoka kileleni hadi kushika nafasi ya tatu.
Aidha, tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi hiyo, Simba imeshinda
mechi mbili dhidi ya African Lyon 3-1 na Tanzania Prisons 1-0, huku
ikitoka sare mbili dhidi ya JKT Ruvu na JKT Oljoro kwa bao 1-1 kabla ya
kufungwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar juzi.