TAARIFA
iliyotua kwenye dawati la gazeti hili hivi karibuni inaeleza kuwa,
mavazi yasiyo ya heshima vikiwemo vimini yamepigwa marufuku...
kuvaliwa
na wasanii kwenye filamu wanazorekodi na yoyote atayekiuka atakiona cha
mtemakuni.Chanzo chetu makini kilichoomba hifadhi ya jina lake,
kimeeleza kuwa waliotoa agizo hilo ni Serikali ya Tanzania kupitia Bodi
ya Filamu lengo likiwa ni kuhakikisha maadili ya taifa yanazingatiwa.
Ikaelezwa
kuwa hatua hiyo imekuja kufuatia uwepo wa filamu nyingi mtaani ambazo
wasanii wanaoshiriki huvaa mavazi yasiyo ya heshima, mazingira
yanayoiharibu jamii.
“Kama
wanavyosema vijana huko mtaani kwamba kimenuka na kweli kimenuka! Sasa
hivi vimini ‘no’ kwenye filamu, bodi ya filamu imeona ilivalie njuga
suala hili ili kulinda maadili ya taifa,” kilieleza chanzo hicho.
Katika
kujua ukweli wa jambo hili, mwandishi wetu alimtafuta Rais wa
Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifwamba ambaye alikiri
kuwepo kwa utaratibu mpya wa Bodi ya Filamu wa kuzipitia filamu
zinazoingia mtaani na kwamba zinazokiuka maadili zinafungiwa.
Mwakifwamba
alisema ni kweli mavazi ya nusu utupu hayataruhusiwa tena kuonekana
kwenye filamu kama ilivyokuwa huko nyuma na wale watakaojifanya vichwa
ngumu watashughulikiwa.
“Sasa
hivi kuna sheria mpya kabisa, hakuna kuvaa nguo zisizo za maadili na
ukikiuka basi filamu yako haioneshwi au kama unaweza urudie na kuondoa
vipande vilivyoharibu filamu hiyo,” alisema Mwakifwamba huku kukiwa na
maelezo kuwa, hilo pia litasimamiwa na Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo chini ya Waziri Fenella Mukangara.