Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewajibu wabunge waliokosoa kitendo cha mawaziri watano waliotajwa kwenye kashfa za Operesheni Tokomeza na akaunti ya escrow, akisema Ikulu haikuhusika kuwasafisha bali ilitangaza matokeo ya uchunguzi wa tume.
Mtendaji huyo mkuu wa Serikali pia amesema mawaziri hao bado wanachunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Jeshi la Polisi, kuhusu kuhusishwa kwao na operesheni hiyo iliyotekelezwa kwa kukiuka haki za binadamu, na sakata la escrow lililohusisha uchotwaji wa Sh306 bilioni zilizokuwa Benki Kuu.
Wakichangia hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu wiki iliyopita, baadhi ya wabunge walihoji kitendo cha Ikulu kuwasafisha mawaziri wachache na kuwaacha wengine waliojiuzulu kisiasa kutokana na wizara zao kukumbwa na kashfa na kumtaka Waziri Mkuu atoe majibu wakati akifanya majumuisho ya mjadala.