Monday, April 30, 2018

MBUNGE CHADEMA ALALAMIKIA VITI BUNGENI, ADAI KUFINYWA MAKALIO

Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) ameomba mwongozo bungeni akitaka viti vya bungeni kukarabatiwa kwa kuwa viti hivyo ni vibovu.

“Ni lini serikali itakarabati viti hivi, hiki nilichokalia leo asubuhi kimenifinya makalio,“ alihoji Selasini.

Salasini ameyasema hayo leo Bungeni mjini Dodoma, wakati wa kipindi cha Maswali na majibu huku akiitaka serikali itoe majibu ni lini viti hivyo vitakarabatiwa.

Aidha Mbunge huyo baada ya kuhoji amesema kuwa kiti alichokalia leo katika bunge hilo kimemfinya makalio. Sambamba na kuomba muongozo huo Spika Ngudai amesema kuwa suala hilo limepokea na litatolewa ufafanuzi.

MAJIBU YA RAIS MAGUFULI KWA WANAOBEZA NCHI KUKOPA

Rais John Magufuli amesema Serikali itaendelea kukopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, hata kama kuna watu wanabeza.

Amesema fedha hukopwa kwa masharti nafuu, riba ndogo na hulipwa kwa muda mrefu na kwamba fedha hizo ndizo hutumika kujenga miundombinu kama barabara ili kuchochea uchumi.

Rais alisema hayo jana mjini Iringa alipofungua barabara ya lami ya Iringa – Migoli – Fufu yenye urefu wa kilomita 189 inayounganisha mikoa ya Iringa na Dodoma. Tukio hilo lilirushwa hewani moja kwa moja na kituo cha televisheni cha TBC 1.

Barabara hiyo iliyojengwa kwa gharama ya Sh207.4 bilioni ni sehemu ya barabara kuu ya kuanzia Cape Town, Afrika Kusini hadi Cairo nchini Misri.

Imejengwa kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa asilimia 65.9, Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (Jica) kwa asilimia 21.3 na Serikali ya Tanzania asilimia 12.8.

“Msiwasikilize wanaosema Serikali ina madeni makubwa wakati wao wenyewe wanapita kwenda bungeni kwenye barabarani tulizozijenga kwa kukopa,” alisema.

Magufuli alisema Serikali imekuwa ikidaiwa tangu enzi za mkoloni, lakini madeni mengine yamekuja kulipwa katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete.

Akizungumzia barabara hiyo, Rais alisema inalenga la kuimarisha utalii katika ukanda wa kusini.

“Watu walizoea (kwamba) ukitaka kutalii ni lazima uende Serengeti wakati Ruaha ni mbuga kubwa yenye vivutio bora, lakini haikutembelewa na watalii kwa sababu ya ukosefu wa barabara,” alisema.

“Kwa sasa itabidi wenzetu wa kaskazini wasubiri kwanza. Kwa sasa tunaendeleza maeneo yaliyochelewa kuendelezwa,” alisema.

Rais Magufuli alisema Uwanja wa Ndege wa Nduli uliopo Iringa utaimarishwa ili watalii waweze kufika maeneo ya utalii.

Rais Magufuli alisema barabara hiyo pia itawasaidia wakazi wa Iringa kusafirisha mazao kwenda sokoni bila matatizo.

“Barabara hii iwe mkombozi wa maisha yetu. Tuitunze, itasafirisha mazao, mtasafiri kwa utulivu kwenda kwenye shughuli zenu,” alisema.

Magufuli ambaye alisoma Shule ya Sekondari Mkwawa mkoani Iringa kuanzia mwaka 1978/79, alisema anakumbuka hali ya barabara ilivyokuwa tatizo wakati huo.

“Kutoka Dodoma hadi Iringa nilitumia siku mbili kwa kutumia basi la Shirika la Reli Tanzania. Tulilala njiani kwa sababu ya ubovu wa barabara,” alisema.

MCHUNGAJI KKKT ADAI KUNA UBABE KATIKA KANISA HILO

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kigogo, Richard Hananja amedai kuna ubabe katika kanisa hilo.

Hata hivyo, amesema licha ya kanisa hilo kupitia mambo mengi anaamini litaendelea kusimama imara hasa katika kipindi hiki.

Mchungaji Hananja amesema hayo Aprili 29, 2018 alipozungumza na Mwananchi kuhusu baraza la maaskofu wa KKKT ‘kuwatenga’ maaskofu watatu kwa kutosoma waraka wa ujumbe wa Pasaka kwenye dayosisi zao.

SERENGETI BOYS MABINGWA WA CECAFA

Timu ya Tanzania ya vijana wasiozidi umri wa miaka 17 Serengeti Boys ndio mabingwa wa Kombe la Vijana la mataifa ya Afrika Mashariki na Kati Cecafa wa mwaka 2018.

Serengeti Boys walitwaa ubingwa baada ya kuwalaza Somalia mabao 2-0 katika mechi ya fainali iliyochezewa mjini Bujumbura, Burundi. Mabao ya Serengeti yalitiwa kimiani na Edson Jeremiah na Japhary Mtoo.

Ushindi huo ndio wa kwanza tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo mwaka 2007 na unatarajiwa kuwatia moyo vijana hao wanapijiandaa kushindi michuano ya Kombe la Vijana Mabingwa Afrika mwaka 2019.

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...