Adaiwa kuuawa Westgate
*Alifika Tanzania kwa Pasipoti ya Afrika Kusini
*Alifika Tanzania kwa Pasipoti ya Afrika Kusini
Ssamantha Lewthwaite, mwanamke wa Uingereza anayetajwa kuwa kiongozi wa ugaidi uliofanyika Nairobi, Kenya
WAKATI umwagaji wa damu katika kituo cha biashara cha Westgate ukiingia siku ya nne jana, Mwanamke ambaye ni raia wa Uingereza, Samantha Lewthwaite (29), anayetajwa kuwa ndiye aliyeongoza kundi la Al-Shabab kufanya shambulizi hilo, anahofiwa kuuawa.
Gazeti la Daily Mail la Uingereza, lilikariri vyanzo vyake vilivyoko ndani ya Jeshi na mfumo wa usalama nchini Kenya, ambavyo vimethibitisha kuwa mwanamke huyo ni miongoni mwa magaidi waliouawa na Serikali ya Kenya.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed, katika mahojiano yake na kituo cha habari cha PBS, hakusema kama mwanamke huyo ameuawa lakini alithibitisha kuwa miongoni mwa magaidi waliovamia Westgate ni mwanamke wa Uingereza ambaye hata hivyo hakumtaja jina.
Hatua hiyo iliibua tetesi kwenye vyombo vya habari vya Kenya ambavyo vilimtaja mwanamke huyo kuwa ni Samantha.
Hata hivyo kauli hiyo ya Waziri huyo inaonekana kupingana na ile iliyotolewa awali na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Kenya, ambaye alisema kuwa magaidi wote waliovamia kituo hicho walikuwa wanaume na kwamba huenda baadhi yao walivalia mavazi ya kike.