Wamiliki wa vituo vyote vya mafuta nchini Tanzania wamepewa siku 14 kufunga na kuanza kutumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti la sivyo wafutiwe leseni.
Rais Magufuli, ambaye ametoa agizo hilo, ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha vituo vyote vya mafuta nchini vinatumia mashine hizo ambazo kwa Kiingereza zinafahamika kama Electronic Fiscal Petrol Printer na kusisitiza kuwa wamiliki watakaokiuka agizo hilo vituo vyao vifungwe na kufutiwa leseni.
"Na kwa hili natoa siku 14, wale wenye vituo vya mafuta wote, uwe upo Chato, uwe Biharamulo, uwe Kagera, uwe Dar es Salaam hakikisha una hiyo mashine, ndani ya siku 14," amesema Dkt Magufuli.
Mwishoni mwa wiki Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) ilivifungia vituo vya mafuta kutokana kutotimiza vigezo baada ya kutofunga mashine za kielektroniki kwenye pampu za mafuta.