Serikali
inapenda kuwaarifu waombaji wa nafasi za kazi kwa tangazo la tarehe 27
Novemba, 2013 wa kada za Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Udereva kuwa usaili
utaanza tarehe 4 Machi, 2014 takriban katika mikoa yote Tanzania Bara na
Zanzibar.
Katibu
wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi
amesema hayo leo ofisini kwake wakati akiongea na baadhi ya wadau
waliomtembelea kwa lengo la kufahamu masuala mbalimbali ya uendeshaji wa
mchakato wa ajira serikalini.
Amesema
usaili huo unaoanza tarehe 4 Machi katika mikoa takribani yote nchini
utahusisha jumla ya wasailiwa 6,087 wa fani za Kilimo, Mifugo, Uvuvi na
udereva kwa kada ambazo sio za Maofisa. Amefafanua kuwa vigezo vya
kupanga mikoa ya usaili vimetokana na anwani ambazo waombaji
waliwasilisha katika barua zao za maombi husika ya kazi.
Daudi
alibainisha kuwa kila mwombaji aliyekidhi vigezo na kuchaguliwa kwa
ajili ya usaili anapaswa kwenda kufanyia usaili katika mkoa aliopangiwa
kama anwani yake inavyoonyesha katika tangazo kwenye tovuti ya
Sekretarieti ya Ajira, isipokuwa kwa waombaji wa mkoa wa Katavi wao
wataenda kufanyia usaili mkoa wa Rukwa na waombaji waliotumia anwani za
mkoa wa Singida wao watafanyia usaili mkoa wa Manyara kutokana na sababu
zisizozuilika.
Aliongeza
kuwa kwa mwombaji ambae hatazingatia anwani, siku na muda aliopangiwa
na kuamua kwenda mkoa mwingine tofauti na utaratibu uliopangwa ajue wazi
hatasailiwa kwa kuwa ratiba na idadi ya majopo ilishapangwa kwa kila
mkoa na haitabadilishwa ili kuweza kurahisisha kazi hiyo kukamilika kwa
ufanisi.