UTAFITI uliofanywa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii unaonyesha kuwa wakazi wa Mkoa wa Dar es salam 6800 tayari wamepata athari ya matende na mabusha.
Akizungumza katika zoezi hilo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dk Grace Magembe alisema mpaka sasa tayari watu 104 kwa Mkoa wa Dar es Salaam wameshafanyiwa upasuaji wa mabusha.
Alisema kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa wa mabusha Jijini Dar es Salaam wanatarajia kuwafanyia upasuaji wagonjwa 1000.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa dawa za kinga tiba ya Matende, Minyoo na Mabusha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, alisema kuwa kiwango hicho ni kikubwa sana kwa wakazi wa dar es salaam kwani mpaka sasa watanzania milioni 2.7 wameathirika na magonjwa yasiyopewa kipaumbele ikiwemo ngiri maji pamoja na matende hususani vijijini.
Alisema zoezi la utoaji wa dawa za kinga tiba litatolewa bure ambapo zaidi ya watanzania milioni 4.5 wanatarajiwa kupata kinga tiba hizo.
“Kinga tiba imeanza kutolewa Oktoba 25 hadi 29 kwa watu wenye umri kuanzia miaka 5 na kuendelea kwa kumeza dawa za Mectizan na Albendazole za kukinga na kutibu magonjwa ya minyoo tumbo,mabusha na matende,” alisema Makonda.