MBOWE ASEMA HUO NI
MTIRIRIKO WA MABAVU YA DOLA
MAHAKAMA ya
Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana ilimfutia kesi ya makosa ya
ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph, kisha
kuwakamata tena na kuwafungulia kesi mpya yenye mashitaka yaleyale.
Awali
ilielezwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka ( DPP), Dk. Eliezer Feleshi,
aliwasilisha hati ya kuwafutia kesi washitakiwa kwa sababu hana haja ya
kuendelea nayo.
Hata hivyo
baada ya kuachiwa, Lwakatare na mwenzake walikamatwa tena na kufikishwa
mahakamani hapo kisha kufunguliwa kesi mpya namba 6/2013 ambayo
imepangiwa kwa Hakimu mpya, Aloyce Katemana.
Katika kesi
ya awali namba 37/2013 iliyofunguliwa na Jamhuri dhidi ya Lwakatare na
wenzake Machi 18, mwaka huu, jana ilikuwa imekuja kwa ajili ya Hakimu
Mkazi, Emilius Mchauru, kuitolea uamuzi wa ama kuwapatia dhamana
washitakiwa hao au la.
Lakini
Hakimu Mchauru alijikuta akishindwa kutoa uamuzi wake kwa
sababu mawakili viongozi wa serikali, Ponsian Lukosi, Prudence
Rweyongeza na Peter Mahugo, waliwasilisha hati hiyo ya DPP chini ya
kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka
2002.
“Kwa kuwa kesi hii Na. 37/2013 ilifunguliwa na
upande wa Jamhuri Machi 18, mwaka huu, na leo kesi hii ilikuja kwa ajili
ya mahakama kutolea uamuzi wa maombi ya washitakiwa kupatiwa dhamana au
la, pamoja na maombi mengine…mahakama hii inasema haitaweza kutoa
uamuzi wake kwa sababu DPP amewasilisha hati ya kutotaka kuendelea
kuwashitaki, hivyo mahakama hii inawafutia kesi washitakiwa wote,”
alisema Hakimu Mchauru.
Baada ya
Hakimu Mchauru kuwafutia kesi, askari kanzu waliwakamata tena
washitakiwa hao na kuwaweka chini ya ulinzi na ilipofika saa 4:20
asubuhi, waliingizwa tena katika ukumbi namba mbili wa mahakama hiyo
mbele ya Hakimu Mkazi mwingine, Aloyce Katemana.