SAA
chache baada ya kufunguliwa kwa Dirisha Dogo la Usajili kwa msimu wa
2013/14, vinara wa Ligi Kuu ya Vodacom, Yanga jana walifanikiwa
kumsajili kwa mkataba wa miaka mitatu kiungo Hassan Dilunga kutoka Ruvu
Shooting ya Pwani.
Kwa
mujibu wa kanuni, klabu za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza zenye fursa ya
kusajili wachezaji katika dirisha dogo ni zile ambazo hazijatumia nafasi
zote 30 za wachezaji, usajili uliofunguliwa jana Novemba 15 na
kutarajiwa kufungwa Desemba 15.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Usajili wa klabu ya Yanga, Abdallah Bin Kleb, alisema jana
kwamba usajili wa kiungo huyo ni utekelezaji wa maagizo ya Kocha Mkuu,
Ernie Brandts, aliyoyaacha na benchi lake la ufundi kwa ajili ya
kuboresha kikosi.
"Kocha
aliacha mapendekezo ya usajili tuyafanyie kazi, la kwanza lilikuwa ni
kuhakikisha tunampata Kaseja ili kuongeza nguvu miongoni mwa makipa,
ambao tuliukamilisha mwishoni mwa wiki na sasa tumelimaliza la kiungo
Hassan Dilunga," alisema Bin Kleb na kuongeza.
Kikubwa
kuhakikisha kuwa, tunatekeleza maagizo yote yaliyo katika ripoti ya
benchi la ufundi na kuyafanyia kazi ili kujiweka katika mazingira mazuri
ya kuboresha kikosi chetu kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na
michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Usajili wa Dilunga kiungo aliyeteuliwa
kikosi cha timu ya taifa, 'Taifa Stars', inayojiandaa kucheza mechi ya
kirafiki dhidi ya Harambee Stars, ametua Jangwani siku chache baada ya
mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu walipomsajili mlinda mlango wa zamani
wa Simba na Stars, Juma Kaseja, aliyekuwa hana timu tangu kumaliza
mkataba wake na Wekundu wa Msimbazi.