Godfrey Mosha |
Mkurugenzi
wa Kampuni ya Principal Ltd, Godfrey Mosha amesimulia jinsi Benki ya
Akiba Commercial (DCB), tawi la Kariakoo, ilivyoidhinisha malipo ya
fedha kwa mtu mwingine kutoka akaunti yake ndani bila yeye kujua.
Mosha
ni mmoja wa washtakiwa katika kesi ya wizi wa fedha kwenye Akaunti ya
Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Pamoja na
wenzake, Bahati Mahenge, Manase Makale, Davis Kamungu na Eda Makale,
wanakabiliwa na kesi ya wizi wa Sh1.86 bilioni za EPA, katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuipitia Kampuni ya Changanyikeni Residential
Complex.
Katika
kesi hiyo dhidi ya DCB, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, Warialwande Lema, Mosha anaidai benki hiyo Sh46.8
milioni, zilizolipwa kwa mtu asiyemfahamu kwa kutumia hundi nne tofauti
na tarehe tofautitofauti.
Katika
ushahidi wake Ijumaa iliyopita, akiongozwa na Wakili wake, Michael
Ngalo, Mosha alidai alibaini uhamisho huo wa fedha kutoka akaunti
yake namba 0400438671, Novemba 15, 2011 alipochukua taarifa ya benki.