Viongozi
wa vyama vikuu vya upinzani nchni kutoka kushoto: James Mbatia (NCCR
Mageuzi), Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahimu Lipumba (CUF).
Viongozi wa vyama vikuu vya upinzani vyenye wabunge bungeni
wanatarajia kukutana leo na Rais Jakaya Kikwete Ikulu, jijini Dar es
Salaam kuzungumzia utata wa baadhi ya masuala yaliyojitokeza katika
mchakato unaoendelea wa kupata Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Kama wengi tunavyotegemea, mazungumzo hayo kwa vyovyote ni ya masuala nyeti ambayo yamesababisha mvutano na kuibua hisia kali miongoni mwa makundi ya kijamii, pengine kwa kutambua fika kwamba kupuuza madai ya wapinzani ingekuwa sawa na kumwaga petroli katika nyumba inayoungua, busara za rais wetu zimemfanya awaite viongozi wa kisiasa kuteta nao Ikulu.
Wakati viongozi hao, Freeman Mbowe wa Chadema, James Mbatia wa NCCR Mageuzi na Profesa Ibrahimu Lipumba wanakutana na kiongozi wa nchi leo, pengine akiwa hajasaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambao ulipelekwa mezani kwake baada ya kupitishwa bungeni na wabunge wa CCM wiki chache zilizopita, watampa mwanga kilichowafanya waugomee bungeni, maana katika hotuba yake alisema ameambiwa hiki na kile sasa atasikia laivu kutoka kwao.