Wakati Tanzania ikisema kuwa iko
tayari kukaa meza moja na jirani yake Rwanda kumaliza hali ya uhasama
iliyoanza kujitokeza katika siku za hivi karibuni, Katibu Mkuu wa
Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Richard Sezibera amesema
jitihada za kidipolomasia zinafanyika kutatua tofauti hizo za
kimawazo.
Bila kutaja taasisi wala wanaohusika katika jitihada hizo za
kidiplomasia, Dk Sezibera aliwaambia waandishi wa habari jijini Arusha
jana kuwa jitihada hizo zinafanyika kimya kimya bila kushirikisha vyombo
vya habari "Migongano na tofauti za kimtazamo miongoni mwa viongozi
wakuu wa nchi wanachama wa EAC ni jambo lisilo la afya kwa Jumuiya na
linastahili kushughulikiwa kidiplomasia," alisema Dk Sezibera.
Akizungumza kwa tahadhari kubwa
kukwepa kuingia kwa undani kuhusu suala hilo, Katibu Mkuu huyo alisema
inafaa kila linalowezekana lifanyike kutatua mgongano wowote unaotokea
kati ya viongozi wakuu.
Mjini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe naye alisema katika
mahojiano kuwa iwapo Rwanda itaomba kukutana na Tanzania kwa ajili ya
kumaliza mzozo huo Serikali itakuwa tayari kutoa ushirikiano.