Waziri wa Ulinzi, Dk Hussein Mwinyi amesema vijana ambao watakaidi wito wa kuhudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria, watakuwa wamekaidi amri halali na majina yao yatapelekwa mamlaka za ajira kwa ajili ya hatua dhidi yao.
Kauli hiyo ameitoa wakati JKT ikiendelea na mchakato wa kufufua kambi tano nchini ili kufanikisha uwezeshaji wa vijana wanaomaliza elimu ya juu ya sekondari kujiunga na jeshi hilo kwa kujitolea na kwa mujibu wa sheria.
Awali, ilikuwa lazima kwa wahitimu wa elimu ya juu ya sekondari na vyuo kujiunga na mafunzo ya mwaka mmoja JKT kabla ya kuendelea na masomo au kuanza ajira, na baadaye muda ukapunguzwa.