Waziri wa Ulinzi, Dk Hussein Mwinyi amesema vijana ambao watakaidi wito wa kuhudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria, watakuwa wamekaidi amri halali na majina yao yatapelekwa mamlaka za ajira kwa ajili ya hatua dhidi yao.
Kauli hiyo ameitoa wakati JKT ikiendelea na mchakato wa kufufua kambi tano nchini ili kufanikisha uwezeshaji wa vijana wanaomaliza elimu ya juu ya sekondari kujiunga na jeshi hilo kwa kujitolea na kwa mujibu wa sheria.
Awali, ilikuwa lazima kwa wahitimu wa elimu ya juu ya sekondari na vyuo kujiunga na mafunzo ya mwaka mmoja JKT kabla ya kuendelea na masomo au kuanza ajira, na baadaye muda ukapunguzwa.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili jana, Waziri Mwinyi amesema uchaguzi wa vijana wanaotakiwa kujiunga na mafunzo hayo unafanyika bila kutumia kigezo chochote zaidi ya kuwa mhitimu wa kidato cha sita.
“Yeyote ambaye jina lake linakuwa kwenye orodha ya wanaotakiwa kuhudhuria mafunzo, ni lazima akahudhurie na asipoenda anakuwa amekiuka amri halali. Majina ya walioteuliwa, yalionyesha waliohudhuria na waliokaidi tunayapeleka katika mamlaka za ajira,” amesema Dk Mwinyi.
Hivi karibuni wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya JKT kwa vijana wa kujitolea katika kambi ya 838 KJ Maramba wilayani Mkinga, Brigedia Jenerali John Mbungo amesema jeshi hilo linakusudia kufufua kambi tano.
Amezitaja kambi hizo kuwa ni 826 Mpwapwa mkoani Dodoma, 845 Itaka (Songwe), 846 na 847 zilizoko Rukwa na 839 Makuyuni (Arusha) ambayo imeshaanza kupokea vijana ambao wanaendelea na mafunzo.
No comments:
Post a Comment