CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO Idara
ya Habari ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), tangu
ilivyopokea kwa masikitiko na mshituko mkubwa taarifa za Serikali ya
CCM, kufungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania, imeendelea kufuatilia
kwa ukaribu hatua zinazochukuliwa na kauli mbalimbali zinazotolewa na
pande zote mbili, serikali na wadau wa uhuru wa habari na vyombo vya
habari.
Ni wazi
bila shaka yoyote kuwa kwa mara nyingine tena, serikali hii, imeendelea
kutumia sheria mbaya, kutumia madaraka vibaya kufanya uamuzi mbaya, kila
inapokosa hoja na uwezo wa kukabiliana na sauti mbadala au maoni
kinzani.
Suala hili limekuwa
dhahiri zaidi baada ya Serikali kuamua hata kuanza kuingilia uhuru wa
habari na maoni kwenye mitandao ya kompyuta (on line) na pia kutishia
kulifungia Gazeti la Rai, linalotolewa na Kampuni ya New Habari (2006)
Limited, kwa sababu limeanza kuchapiswa kila siku.
Wakati
wamiliki wa gazeti hilo wametoa ushahidi unaotokana na nyaraka za
serikali hiyo hiyo iliyotoa idhini kwa chombo hicho kuchapishwa kila
siku, Serikali yenyewe kwa upande wake imetoa utetezi wa ajabu juu ya
tishio lake hilo ikijitetea kuwa kibali hicho kilitolewa kwa Kampuni ya
Habari Corporation iliyouza hisa zake kwa Kampuni ya New Habari (2006)
Limited.
Katika hili serikali
inajichanganya. Hii ni dalili ya wazi kwamba uamuzi wake huo ni
mwendelezo wa maamuzi ya kibabe, yasiyofanywa kwa masilahi ya
Watanzania, ndiyo maana yanaanza kuipatia tabu jinsi ya kujibu na
kujenga hoja za kutetea uovu wake.
CHADEMA, inapinga na itaendelea kupinga kwa kauli na vitendo, hatua hii ya serikali yenye lengo ovu dhidi ya umma wa Watanzania.