Mabomu ya machozi yalipigwa ili kuzuia wafanyabiashara wasilete vurugu
Maduka yakiwa yamefungwa
Wafanyabiashara hao walichoma matairi ili kuwazuia polisi wasiweze kuwafikia
Na Kenneth Ngelesi
WAFANYABIASHARA mkoani Mbeya wamezua
kizaazaa wakigoma kufungua maduka wakipinga agizo la Mamlaka ya Mapato
nchini (TRA) linalowataka kununua mashine za kielektroniki kwa ajili ya
kukatia risiti za wateja pindi wanapowauzia bidhaa.
Katika sokomoko hilo lililotokea jana
na kusababisha taharuki kwa muda kadhaa, wafanyabiashara hao wanadai
kuwa gharama za mashine zitolewe na serikali.
Eneo la Soko la Sido ambalo lina
wafanyabiashara wengi na tegemeo katika uchumi wa Jiji la Mbeya,
walifunga biashara zao kwa muda usiojulikana.
Kadhia hiyo inakuja siku moja tangu
Mkuu wa Mkoa huu, Abbas Kandoro, akutane na viongozi wa wafanyabiashara
kutoka Soko la Sido na kuwataka viongozi kuwataarifu wenzao wasitishe
mkutano ambao walitaka kuufanya jana katika uwanja wa Shule ya Msingi
Ruanda Nzovwe.
Kandoro alifikia uamuzi wa kukutana na
viongozi hao baada ya kupata taarifa kupitia gari la matangazo ambalo
lilikuwa likipita na kuzunguka katikati ya jiji na kuwataka
wafanyabiashara hao kufunga maduka na kufika mkutanoni ili kujadili
suala zima la mashine hizo.
Taarifa zinadai kuwa baada ya Kandoro
kusikia matanagzo hayo, aliliagiza Jeshi la Polisi kumkamata dereva wa
gari hilo pamoja na Mwenyekiti wa Soko la Sido na kuwaweka rumande kwa
muda usiojulikana.
Baada ya wawili hao kuwekwa ndani,
lilitolewa agizo la kuzunguka tena mitaani kwa kutumia gari hilo ili
kuwatangazia wafanyabiashara hao kuwa mkutano huo umesitishwa.
Uamuzi wa kusitisha mkutano huo
ulipuuzwa na wafanyabiashara hao ambao jana waliendelea na maandilizi
ikiwa ni kukodi gari jingine la matangazo kupita mitaani kuwahimiza
wenzao kujitokeza kwa wingi. Hatua hiyo iliufanya uongozi wa mkoa
kuwasambaza polisi mitaani kuzuia mkutano huo. Mabomu ya machozi na maji
ya kuwasha vilitembezwa kwa wafanyabiashara hao ambao walikuwa
wamekusanyika huku maduka yao yakiwa yamefungwa.
Mabomu hayo ya polisi yaliwaathiri
wanafunzi wa Shule ya Msingi Kagera na kuwafanya wataharuki na kuanza
kukimbia hovyo huku wengine wakizirai.
Kufuatia hali hiyo, Mwalimu Mkuu wa
shule hiyo, Ayoub Kiwanga, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ilomba, Erasto
Mwakaponda na Diwani wa kata hiyo, Dickson Mwakilasa, walikubaliana
kuwakabidhi wanafunzi hao kwa wazazi wao waliofika shuleni hapo
kuwajulia hali baada ya kupokea taarifa za kupigwa mabomu.
Wakizungumza na Tanzania Daima,
wafanyabiashara hao walisema kuwa wanashindwa kuelewa nguvu kubwa ambayo
inatumiwa na polisi wakati hakuna vurugu zozote katika eneo hilo.
Alex Oswald, kwa niaba ya wenzake
alisema kuwa wao waliamua kufunga maduka kwa hiari yao na kwamba lengo
la mkutano lilikuwa kutoa msimamo wa kuiomba serikali itoe mashine hizo
bure.
Naye Peter Tweve, alisema kuwa
kimsingi wao hawajagoma kutumia mashine hizo bali wanataka wawekewe
bure, kwani si kila mfanyabiashara anaweza kuinunua mashine hiyo ambayo
kwa sasa inauzwa kwa sh 800,000.
Alipotafutwa Kandoro kuelezea tukio
hilo, aligoma akisema kuwa yupo katika kikao, pia Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, simu yake iliita bila kupokewa.
Wiki moja iliyopita, Mkurugenzi wa
Elimu ya Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alitoa taarifa kuwa
wafanyabiashara wenye mapato ya zaidi ya sh 45,000 kwa siku wanapewa
hadi Oktoba 14, mwaka huu wawe wamenunua mashine hizo.
No comments:
Post a Comment