Siku
chache baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto
Kabwe kutaja hadharani mishahara ya Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, serikali imekataa kuizungumzia mishahara hiyo.
Msimamo
wa Serikali kutotaja mishahara ya viongozi wakuu unatofautiana na
utamaduni wa nchi nyingine kama Marekani, Afrika Kusini, Ufaransa na
Kenya ambazo mishahara ya wakuu wake huwekwa wazi kwa umma.
Zitto
ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema akiwa wilayani Igunga Mkoani
Tabora, alisema Rais Kikwete anapokea zaidi ya Sh30 milioni kwa mwezi
(sawa na Sh360 milioni kwa mwaka) ikiwa ni marupuru na mshahara kwa
mwezi bila kodi, huku Pinda akipokea Sh 26 milioni kwa mwezi.
Akizungumza
na Mwananchi kwa simu jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti
ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani alisema kiongozi yeyote haruhusiwi
kutaja mshahara wa mtu mwingine kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha
sheria ya utumishi wa umma.
"Kuutaja
mshahara wa mtu mwingine ni kinyume cha sheria na kosa, siyo utaratibu.
Kwani wewe upo tayari watu waujue mshahara wako?" alihoji.