MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini, Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba, ametetea muundo wa serikali tatu kuwa hauna gharama, tofauti na inavyotafsiriwa na wengi. Mbali na kutetea gharama za uendeshaji wa serikali tatu, Jaji Warioba pia amewashukia wanaodhani mapendekezo ya muundo wa serikali tatu ni yake binafsi, kutokana na msimamo wa siku nyingi wa kiongozi huyo.
Akizungumza na Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Jaji Warioba alisema muundo wa serikali tatu umepunguza gharama za uendeshaji. Kwa mujibu wa Jaji Warioba, chini ya muundo huo hata Bunge linatarajiwa kuwa na wabunge 75 tu, hatua ambayo itapunguza gharama. Mwenyekiti huyo alisema kuwa gharama za uendeshaji wa Serikali ya Muungano zitakuwa katika Wizara ya Ulinzi na Usalama pamoja na Mambo ya Nje huku katika maeneo yaliyobaki gharama zake zitakuwa zimepungua zaidi.
“Hivi kwa nini hili la muundo wa muungano tunajadili gharama wakati kila mwaka tunapoongeza mikoa, wilaya, tarafa, majimbo na vijiji gharama zinaongezeka wala hakuna anayezungumzia wala kuhoji? Hivyo hivyo kwa kuwa na serikali tatu, hakuna gharama, tena kimsingi tumepunguza gharama za migogoro ya mara kwa mara ya kushughulikia kero za Muungano,” alisema Jaji Warioba.