Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa sarafu maalumu ya kumbukumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye thamani ya sh 50,000.
Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, alisema jana kuwa sarafu hiyo
iliyotengenezwa kwa madini ya fedha kwa asilimia 92.50, imetolewa kwa
ajili ya kumbukumbu tu na haitaingizwa katika mzunguko wala kutumika kwa
kulipia malipo ya aina yoyote.
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz
Sarafu hii imetolewa maalumu kama maadhimisho ya miaka 50 ya mapinduzi ya Zanzibar, haitatumika kwa manunuzi.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Idara ya Uhusiano wa
Umma na Itifaki ya BoT ilimnukuu Profesa Ndulu akisema sarafu hiyo
imetolewa kwa idadi ya vipande 3,000 kwa ajili ya tukio hilo na
kuwahimiza wananchi kuinunua kwa ajili ya kumbukumbu hiyo.
Kwa mujibu wa Gavana, kutolewa kwa sarafu hiyo kunakwenda sambamba na
utaratibu wa Benki Kuu kutoa sarafu maalumu za aina hiyo kama sehemu ya
maadhimisho ya kumbukumbu ya matukio mbalimbali muhimu ya kitaifa na
kimataifa.
“Kwa kawaida, baada ya muda, thamani ya sarafu kama hizi huongezeka na
kuwa na faida zaidi kwa wanaozimiliki,” alisema Profesa Ndulu.
Gavana Ndulu alieleza sarafu hizo zitapatikana Januari 5 kwa bei ya sh
50,000 katika matawi ya benki za biashara zitakazokuwa zimepata sarafu
hizo kutoka Makao Makuu ya Benki Kuu, Dar es Salaam na matawi ya Benki
Kuu yaliyoko Zanzibar, Arusha, Mbeya na Mwanza.
“Benki za biashara zinaweza pia zikasambaza sarafu hizi kupitia matawi
yake,” alisema gavana na kuongeza taarifa za usambazaji zitatolewa na
benki hizo.
Katika sarafu hiyo, upande wa mbele unaonyesha sura ya hayati Sheikh
Abeid Aman Karume na maandishi yanayosomeka: ‘Rais wa Kwanza wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi’.
Upande mwingine wa sarafu unaonyesha nembo ya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, maandishi yanayosomeka: “Miaka Hamsini ya Mapinduzi”, thamani
ya sarafu na miaka 1964-2014.
Source -Tanzania daima
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz
No comments:
Post a Comment