Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia jana walitofautiana bungeni kuhusu tuhuma za ubadhirifu wa fedha zinazomkabili Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Hadija Nyembo.
Tukio hilo lilitokea baada ya swali la nyongeza la mbunge huyo, aliyetaka kujua msimamo wa serikali kuhusu Nyembo aliyedai kutoa kauli ya kutaka Wabembe waende kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) iliyosababaisha Wabembe kukamatwa na kupelekwa ubalozini, ambapo ubalozi wa DRC , uliwakataa na kusababisha wanyanyasike kwa karibu wiki mbili.
Pia Mbunge huyo alidai Mkuu huyo wa Wilaya aliondolewa wilayani Chato akihusishwa na ufisadi wa mbolea yenye thamani ya Sh bilioni 1.5 na kwamba sasa ana kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Chato, hivyo serikali haioni aibu kuwa na Mkuu wa Wilaya wa aina hiyo, ambaye anashitakiwa na serikali yenyewe.