********
Bunge limepitisha azimio la kuwataka mawaziri katika Ofisi ya
Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kujipima
iwapo wanatosha kuendelea kuongoza wizara hiyo nyeti.
Azimio hilo lilipitishwa jana na wabunge kwa kura
ya ndiyo bila kupingwa, baada ya kuhojiwa na Spika wa Bunge Anne Makinda
iwapo wanaipokea taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(Laac) iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake Rajabu Mbaruku.
Moja ya mapendekezo yake ni Waziri wa Tamisemi,
Hawa Ghasia na manaibu wake, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa kujipima
kama wanatosha kuendelea kuongoza wizara hiyo kutokana na kugubikwa na
vitendo vya ufisadi.
Kwa mujibu wa taratibu za Bunge, taarifa ya kamati
inapowasilishwa na kupitishwa pamoja na mapendekezo yake, huwa ni
azimio kamili ambapo Serikali hutakiwa kutoa maelezo ya utekelezaji
wake.
Kabla ya azimio hilo kupitishwa, Mwenyekiti wa
Laac, Rajabu Mbaruku alijibu michango ya wabunge waliochangia katika
taarifa ya kamati yake iliyowasilishwa Ijumaa iliyopita, akiwemo Waziri
Ghasia.