********
Bunge limepitisha azimio la kuwataka mawaziri katika Ofisi ya
Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kujipima
iwapo wanatosha kuendelea kuongoza wizara hiyo nyeti.
Azimio hilo lilipitishwa jana na wabunge kwa kura
ya ndiyo bila kupingwa, baada ya kuhojiwa na Spika wa Bunge Anne Makinda
iwapo wanaipokea taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(Laac) iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake Rajabu Mbaruku.
Moja ya mapendekezo yake ni Waziri wa Tamisemi,
Hawa Ghasia na manaibu wake, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa kujipima
kama wanatosha kuendelea kuongoza wizara hiyo kutokana na kugubikwa na
vitendo vya ufisadi.
Kwa mujibu wa taratibu za Bunge, taarifa ya kamati
inapowasilishwa na kupitishwa pamoja na mapendekezo yake, huwa ni
azimio kamili ambapo Serikali hutakiwa kutoa maelezo ya utekelezaji
wake.
Kabla ya azimio hilo kupitishwa, Mwenyekiti wa
Laac, Rajabu Mbaruku alijibu michango ya wabunge waliochangia katika
taarifa ya kamati yake iliyowasilishwa Ijumaa iliyopita, akiwemo Waziri
Ghasia.
Akizungumza baadaye, Mbaruku alisema hayo ndiyo
mapendekezo na Serikali itatakiwa kuyatolea maelezo ya jinsi
yatakavyotekelezwa. “Hata waziri mkuu nimemtaja kwa jina, na
nimesisitiza kama ananisikia kuhusu ofisi yake,” alisema.
Katika mchango wake, Waziri Ghasia alijaribu
kupangua tuhuma mbalimbali zilizoelekezwa katika wizara yake ikiwamo
kuwapo ufisadi, ubadhirifu na mtandao wa wizi unaohusisha Hazina, Wizara
na Halmashauri.
Ghasia alikiri Halmashauri ya Mbarali ilitumiwa fedha kuliko kiwango kilichoidhinishwa na Bunge na kwamba
suala la halmashauri mbili za Tanga kupewa zaidi
ya Sh2 bilioni haikuwa sahihi bali yalikuwa ni makosa ya Mkaguzi Mkuu wa
Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kuhusu ufisadi wa zaidi ya Sh600 milioni
zilizotolewa na wafadhili kwa ajili ya mpango wa maboresho ya Serikali
za Mitaa, alisema haamini kama maneno yaliyonukuliwa na vyombo vya
habari kuhusu fedha hizo yalisemwa na wafadhili.
Wafadhili wa mradi huo walinukuliwa wakilalamikia
ufisadi huo na kudai kwa sasa hawana la kufanya na wanamwachia Rais,
huku wakieleza kushangazwa na Rais kuteua watu dhaifu kuendesha wizara
nyeti kama Tamisemi.
Kuhusu hilo, Ghasia alisema hadhani maneno hayo ni
ya wafadhili akisema ni majungu, ni maneno ya waandishi kwa sababu huwa
wanatafuta mambo yanayogusa jambo fulani ili kuuza magazeti.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment