Winnie Madikizela-Mandela, (77) aliinama kumbusu Graca Machel
(68), kabla ya kukaa katika kiti cha tatu kutoka kile alichokalia
mwanamke huyo. Graca Machel alimwambia maneno machache ‘dada yake’
Winnie wakati akimbusu.
Wanawake hao wote wakiwa wamevalia majaketi meusi
na vilemba, walikumbatiana kwa sekunde kadhaa huku Winnie akitabasamu na
Graca akitazama mbele.
Wote wawili wanaheshimika nchini Afrika Kusini
kutokana na sababu mbalimbali. Winnie anaheshimika kwa mchango wake
mkubwa wa kupigania ubaguzi wa rangi; Graca kwa moyo wake wa kujitolea
kumtunza kiongozi wao mpaka anafariki dunia.
Hata hivyo Winnie amekuwa akikosolewa kutokana na
sababu mbalimbali ikiwamo ile ya kuruhusu wapinzani wake wauawe kwa
kuchomwa moto wakitumia mafuta ya petroli na matairi ya magari.
Mwaka 1988 alipatikana na hati ya kumuua kijana wa
miaka 14 ambaye ilidaiwa alimtuhumu kuwa kibaraka, hata hivyo hukumu
yake ilipunguzwa kutoka kuwa kifungo cha miaka sita jela na kuwa faini.
Winnie pia anatuhumiwa kwa kutokuwa mwaminifu
katika ndoa yake iliyodumu kwa miaka 38 ingawa 27 kati ya hiyo hakuwa na
mumewe ambaye alikuwa akitumikia kifungo katika gereza la Robben.
Graca Machel alifunga ndoa na Mandela wakati wa
sherehe yake ya kutimiza miaka 80. Pamoja na kuwa Winnie na Mandela
walitengana, katika kipindi cha ugonjwa wake kilichodumu kwa siku 181,
alikuwa akimtembelea mara kwa mara.
Mjane wa Mandela, Graca, ambaye pia ni mjane wa
Rais wa zamani wa Msumbiji, Hayati Samora Machel, alitumia muda wote
kuwa pembeni mwa kitanda cha Mandela mpaka alipokata roho.
Ndugu wa karibu wanasema, daktari aliposema hakuna
kitu kinachoweza kufanyika kuokoa uhai wa Mandela, Winnie alifika
nyumbani hapo na alikuwepo muda wote mpaka kiongozi huyo alipokata roho.
Tangu Mandela afariki, Winnie amekuwa akionekana
sana tofauti na Graca. Jumapili ya wiki iliyopita, ikiwa ni siku tatu
tangu Mandela afariki, Winnie alikwenda kusali katika kanisa ambalo
lilikuwa likifanya misa kuu ya kitaifa kumuombea Mandela .
Winnie alikaa pembeni ya Rais Jacob Zuma. Hata
hivyo siku yake iliharibia na Mchungaji, Mosa Sono aliyekuwa akiongoza
ibada hiyo baada ya kumtambulisha kwa jina la Graca. Kwa upande wake
Graca alisali katika kanisa dogo lililopo karibu na nyumba ya Mandela.
NA MWANANCHI
TAFADHALI Like ukurasa wetu wa facebook uwe wa kwanza kupata habari bofya/ click HAPA
No comments:
Post a Comment